Kocha wa washambuliaji wa Azam FC, Kally Ongala amewachana washambuliaji wa timu hiyo akisema kukosa umakini wanapokuwa kwenye lango la timu pinzani ndio changamoto inayomtesa, japo anaendelea kupambana ili wafanye kile anachowalekeza uwanja wa mazoezi kuisaidia timu.
Azam juzi usiku ilishinda bao 1-0 mbele ya KMC katika mechi ya Ligi Kuu na kufikisha pointi 47 na kujikita nafasi ya tatu, huku ikipoteza nafsi nyingi na Kally alisema ana kazi kubwa kuweka mambo sawa kwani timu hiyo washambuliaji wengi wakali na wenye uzoefu, lakini bao ni machache.
Akizungumza kocha huyo alikiri Azam ina washambuliaji wengi na wazuri lakini wanakosa umakini wakiwa ndani ya 18 kitu kinachoiangusha timu hiyo yenye mabao 39 katika mechi 24 na ikiruhusu nyavu zao kuguswa mara 24 hadi sasa. Kinara wa mabao wa timu hiyo Idris Mbombo mwenye saba, Prince Dube ana sita, Abdul Suleiman 'Sopu' ana matano na Idd Seleman 'Nado' akiwa na mabao matano.
"Hili ni suala ambalo limekuwa likijirudia kila mara tofauti na tunapokuwa mazoezini, kama benchi la ufundi tutahakikisha tunakaa na wachezaji kujua shida ni nini, ili mambo yaende sawa. Kama kocha nimekuwa ikifanya kazi yangu kwa ukamilifu, lakini tukija uwanjani mambo huwa tofauti," alisema Kally aliyewahi kutamba na timu za Abajalo, Yanga na Azam na kuongeza;
“Kwa juzi Azam tulistahili ushindi tuliopata, kwani timu ilicheza kwa ushirikiano na tulipambana mwanzo mwisho, ila kwa washambuliaji wamekuwa na shida, wametumia nafasi moja tu."
Kallya alisema ataendelea kukaa na washambuliaji kujua nini kinawafanya washindwe kufunga mabao mengi pamoja na kutengeneza nafasi nyingi huku akithibitisha kuwa timu imepewa mapumziko kwa siku tatu watarudi kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (FA).
Timu hiyo intarajiwa kuwa wenyeji wa Mapinduzi ya Zanzibar katika mechi ya 16 Bora itakayopigwa Jumapili Uwanja wa Azam Complex, huku mechi nyingine za hatua hiyo zikianza Alhamisi kwa Simba kuikaribisha Africans Sports na Ijumaa Yanga itakuwa na wenyeji wa Tanzania Prisons na Geita kuvaana na Green Warriors.