Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kally: Heshima inarudi Azam FC

Azam FC Kali Ongala Kally: Heshima inarudi Azam FC

Fri, 4 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kupata ushindi wa pili mfululizo Kaimu Kocha Mkuu wa Azam, Kally Ongala amesema ni suala la muda tu kwao kuheshimika.

Kauli ya Ongala inajiri baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ihefu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Oktoba 31 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi ikiwa ni wa pili kufuatia awali kuifunga Simba 1-0.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kally alisema licha ya wengi kutowapa nafasi ya kufanya vizuri kama timu nyingine kubwa nchini ila hilo kwao haliwatishi kwani watahakikisha wanaendelea kuonyesha ubora wao.

“Hatuwezi kujibu kila mtu anayeongea juu ya kile anachokiamini au kukiona, jukumu letu kubwa ni kuhakikisha timu yetu inaleta changamoto kwa kila mpinzani wetu na hilo linawezekana kutokana na morali iliyopo hapa,” alisema.

Kally aliongeza kitu pekee kinachowafanya kubadilika tofauti na mwanzo ni kila mmoja kufanya majukumu yake ipasavyo kuanzia wachezaji, benchi la ufundi, mashabiki pamoja na hamasa ya viongozi wao.

Akizungumzia hali ya majeruhi, daktari wa kikosi hicho, Mwanandi Mwankemwa alisema kiungo Abdul Suleiman ‘Sopu’ atakaa nje ya uwanja kwa wiki mbili baada ya kufanyiwa vipimo vya MRI na kugundulika kuchanika nyama za paja.

“Tumempa mapumziko hayo, lakini ataendelea kuwa chini ya ulinzi wa madaktari huku akiendelea kufanya mazoezi yake binafsi,” alisema. Nyota huyo aliyesajiliwa msimu huu akitokea Coastal Union alipata majeraha hayo dakika ya tatu ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Akhdar ya Libya uliopigwa Oktoba 16 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Chanzo: Mwanaspoti