Kipa mpya wa Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya anaamini hali anayokutana nayo ni suala la muda na atakaa sawa na kuaminika kikosini.
Kakolanya aliyekuwa Simba, ndani ya Singida alicheza mechi za Ngao ya Jamii katika mechi mbili dhidi ya Simba iliyotoka suluhu na kufungwa penalti 4-2, kisha kulala 2-0 mbele ya Azam FC na tangu hapo amepigwa benchi akianzishwa Benedict Haule aliyekuwa na timu hiyo tangu msimu uliopita.
Haule katika mechi mbili alizodaka ikiwamo ile ya CAF dhidi ya JKU ilishinda 4-1 na ile ya ligi ilitoka suluhu na Tanzania Prisons, huku kukiibuka maswali juu ya nafasi za Kakolanya ndani ya Singida tofauti na matarajio ya wengi kuona kipa huyo akiwa ndiye kipa namba moja naye akavunja ukimya.
Akizungumza nasi, kipa huyo wa zamani wa Yanga na Tanzania Prisons, alisema; “Nina jukumu moja mbele yangu la kucheza vizuri na kupata nafasi ili kujibu maswali ya watu waliokuwa wanajiuliza itakuaje mimi nitakapoanza kuitumikia timu hii. Ni mapema mno kuanza kuhoji nafasi yangu, kila kipa hapa ni nzuri na mtu atapata nafasi kwa kujituma mazoezini, tusubiri.”
Kocha wa Singida, Hans Pluijm amesema kuwa suala la Kakolanya mashabiki wavute subira.