Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kakolanya kusepa Singida Big Stars

Kakolanya.jpeg Kakolanya kusepa Singida Big Stars

Tue, 28 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika kuhakikisha wanaendelea kuiboresha safu yao ya ulinzi, uongozi wa Singida Big Stars upo mstari wa mbele katika mbio za kuinasa saini ya kipa namba mbili wa Simba, Beno Kakolanya, imefahamika.

Singida Big Stars tayari wameanza mchakato huo baada ya msimu huu kupata wakati mgumu katika eneo la kipa na tayari ikielezwa wameweka dau nono mezani kwa Kakolanya, ambaye mkataba wake umebaki miezi minne kufikia ukingoni.

Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana kutoka kwa kigogo mmoja wa Singida Big Stars, zimeeleza kuwa Kakolanya amewekewa mezani mkataba wa miaka miwili na dau la Sh. milioni 100 kama ada ya usajili huku klabu hiyo ikiwa tayari kumlipa mshahara kiasi Sh. milioni tano kila mwezi.

Mtoa habari huyo alisema hatua hiyo ni baada ya wiki iliyopita Kakolanya kukutana na Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula, kwa ajili ya mazungumzo ya kumwongezea mkataba huku ikidaiwa kuwa aliwekewa mezani Sh. milioni 50 kwa ajili ya kusaini mkataba na mshahara milioni sita kwa mwezi.

“Ni kweli Kakolanya mkataba wake uko ukingoni na Singida Big Stars wanahitaji huduma ya kipa huyo na wanahitaji kusaini mkataba wa awali wa miaka miwili kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao.

"Hatua hiyo ya kuhitaji huduma ya kipa huyo wa Simba ni baada ya kuondoka kwa Metacha Mnata kwenda Yanga na Singida Big Stars kukosa mwingine wa uhakika, hivyo wanaimani na uwezo wa Kakolanya,” alisema mtoa habari huyo huku akiomba hifadhi ya jina lake.

Baada ya Kakolanya kutafutwa, alikiri mkataba wake kufikia ukingoni na kwamba ni kweli amepokea ofa ya timu mbili moja ya ndani na nyingine ya nje, kutoka Saudi Arabia.

Alisema kabla ya kufanya mazungumzo na klabu hizo, kwa sasa wanaendelea na mazungumzo na uongozi wa Simba ambao ni waajiri wake wa sasa na kwamba wameonyesha nia ya kuendelea kuhitaji huduma yake.

“Mkataba wangu na Simba umebaki miezi minne kufikia tamati na tupo kwenye mazungumzo na uongozi wangu ambao ninawapa kipaumbele kwa sasa kabla ya kwenda kuzungumza na klabu zingine,” alisema Kakolanya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live