Siku chache baada ya Kamati ya Nidhamu ya Singida Fountaine Gate kumuandikia barua kipa wao, Beno Kakolanya kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazomkabili za kutoroka kambini na kuihujumu timu, staa huyo ameitikia wito huo, lakini amekataa kuhudhuria kikao.
Kwa mujibu wa Singida Fountaine Gate, Kakolanya amejibu barua ya wito kuwa hataweza kufika kwenye kikao cha kamati kwa sababu anahisi kamati haitamtendea haki wakati tayari ameshatuhumiwa.
Akizungumza Ofisa Habari wa Singida Fountaine Gate, Hussein Massanza amesema Kakolanya amejibu barua kwa kukataa wito, hivyo suala hilo wameiachia kamati kutoa uamuzi.
“Lengo la wito wa Kamati ya Nidhamu ni kumuita kujibu tuhuma hizo. Kwa hiyo suala la yeye kukataa wito tunaliacha kwenye uamuzi wa kamati tuone itaamuaje,” amesema Massanza.
Ijumaa ya Aprili 19, mwaka huu, Kamati ya Nidhamu ya Fountain Gate FC ilitakiwa kukutana na Kakolanya baada ya kumuandikia barua ya wito Aprili 14, 2024.
Inadaiwa kwamba, Kakolanya alitoroka kambini muda mfupi kabla ya mechi ya Ligi Kuu kati ya Singida Fountain Gate dhidi ya Yanga iliyochezwa Aprili 14, 2024 na timu yake kukubali kichapo cha mabao 3-0.