Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaheza: Ajali ya Polisi ilinitoa kwenye reli

Kaheza Polisi Kaheza: Ajali ya Polisi ilinitoa kwenye reli

Tue, 17 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba na Yanga ni dili kubwa kwa wachezaji wanaobahatika kuzitumikia, ndivyo anavyoeleza aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Marcel Kaheza akitoa ushuhuda wa maisha aliyoisha akiwa na Wanamsimbazi.

Katika mahojiano ya mchezaji huyo na Mwanaspoti anafunguka namna ambavyo thamani za wachezaji zinavyokuwa kubwa wakiwa kwenye klabu hizo, tofauti na wakiondoka ama kabla ya kujiunga nazo.

Kaheza anaeleza: "Simba na Yanga zinachangia thamani kubwa ya wachezaji heshima zao kupanda mbele ya jamii, kiuchumi kupiga hatua, mfano mzuri kuna huduma nilikuwa nazipata kirahisi sana wakati nipo Simba," anasema na kuongeza;

"Lakini ukiondoka inabakia historia ya jina, mambo mengine yanaondoka, labda uwe umekaa kwa muda mrefu na kufanya mambo makubwa ambayo yataishi kwenye akili za watu, ndio maana utawasikia kocha Abdallah Kibadeni, Edibily Lunyamila, Zamoyoni Mogella na wengine wengi, inamanisha hao wazee wetu walifanya vitu vikubwa."

Simba ilimpa nyumba

Kaheza licha ya kucheza miezi sita baada ya kusajiliwa Simba kwa mkataba wa miaka miwili, akitokea Majimaji ya Songea ambako msimu wa 2018/19, alimaliza na mabao 14, alipiga hatua ya kimaisha.

"Nilifanikiwa kununua kiwanja na kujenga nyumba na kufanya vitu tofauti, hivyo Simba imeniachia alama kubwa kwenye maisha yangu,ingawa kujulikana kuna changamoto na hasara, mfano baada ya kutoka kwa mkopo wengi wao walikuwa wananiona nililewa sifa.

"Ukweli nilisajiliwa kipindi ambacho kilikuwa na ushindani mkali wa namba palikuwa na Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, Clatous Chama hao watu nilikuwa nacheza namba zao, ilinibidi nitolewe kwa mkopo kwenda AFC Leopards ya Kenya kwa mwaka mmoja, kisha nikaenda kumalizia mkopo Polisi Tanzania kwa miezi sita."

Baada ya kufanya vizuri kwa mkopo wa miezi sita, aliongezwa mkataba mwingine wa mwaka mmoja ",Maisha mengine yaliendelea na msimu wa kwanza Polisi Tanzania nilifunga mabao tisa, uliofuata maana nikaongezwa tena mkataba mwingine ambapo nikafunga saba."

Anasema kitu kilichomtoa kwenye ramani ya ushindani ni baada ya kupata ajali akiwa na Polisi Tanzania, Julai 9, 2021 ambapo mfupa wa goti la kulia ulipasuka, hivyo hakuwa na ufiti wa kucheza kwa ushindani na ni ajali iliyomvunja miguu Gerald Mathias Mdamu.

"Ilinisumbua sana na kunikalisha nje kwa muda mrefu, baada ya hapo nikapata nafasi ya kucheza Ruvu kwenye mazoezi nikajitonesha ikanifanya nikae msimu mzima nje, hizo ni changamoto tunazokumbana nazo wachezaji," anasema.

Kwa sasa hana timu, anatoa sababu ya kukaa nje kwamba alisaini na mkataba mmoja na Lipuli ya Iringa, ila changamoto ilikuwepo kwenye uhamisho wa majina, kutokana na uhamisho wa baadhi ya wachezaji kutoka Ruvu Shooting inayocheza Championship.

"Niliambiwa nitajiunga na timu kwenye dirisha dogo, lakini ni moja ya changamoto kubwa kukaa nje ya kazi, kwanza nilizoe kukaa kambini, sasa huku ni kama naanza kuwazoea watu upya,"anasema.

Maxi, Chama ni balaa

Anawataja mastaa wawili Clatous Chama wa Simba na Maxi Nzengeli wa Yanga, namna ambavyo wanaufanya mpira uwe rahisi, kulingana na aina ya uchezaji wao.

"Chama anajua afanye kitu gani akiwa na mpira, anatuliza timu kifupi ana akili kubwa sana, kwa upande wa Maxi anajitolea sana kwa ajili ya timu, anapatikana maeneo mbalimbali uwanjani, kabla mpira haujamfikia anajua ni kitu gani akifanye,"anasema.

Aikumbuka Simba B

Anasema wakati yupo Simba B, wakiwa kwenye harakati za kupandishwa alikwenda kucheza ndondo ambako aliumia na kupata majeraha yaliyomuweka nje miezi sita, wenzake wakapandisha.

"Ilikuwa 2012 wenzangu wakapandishwa nikaja nikapanda dirisha dogo,walikuwa kina Said Ndemla, Jonas Mkude, Ramadhan Singano, Edward Christophe na wengine wengi, tukio hilo liliniumiza sana, maana kwenye ndondo ni hatari mara refa kaingia na panga,"anasema.

Kifo cha Mobby

Anasema hakuna beki aliyekuwa anamkubali kama marehemu Iddy Mobby,anayemuelezea alikuwa na nidhamu, bidii na hamasa kwa wengine.

"Siku moja kabla ya kifo chake alinipigia simu na tuliongea vitu vingi, jambo kubwa ninalolikumbuka alikuwa anasisitiza fanya kazi yako kwa bidii, kutopenda sifa na kujipendekeza, kufanya vitu vitakavyoishi baadaye hata baada ya kuondoka duniani,"anasema.

Jambo kubwa alilojifunza kwenye maisha ya karia yake ni kuyaandaa maisha baada ya kustafu soka, ambayo hayakwepeki na kujenga upendo kwenye familia.

"Kucheza kuna mwisho ila jamii haina mwisho wala familia, kuna haja ya kuvipa kipau mbele vitu hivyo kwa sababu kuna wakati tutavihitaji zaidi,japokuwa sijaoa ila natarajia kumuoa mwanamke niliyezaa naye watoto wawili mapacha wa kike na wa kiume, wana miaka miwili,huwa naliheshimu sana jambo hilo najua kuna kesho,"anasema.

Chanzo: Mwanaspoti