Baada ya kuzagaa kwa taarifa kwamba nyota wa Singida Fountain Gate, Yusuf Kagoma amesaini klabu mbili tofauti za Simba na Yanga, kiungo huyo amevunja ukimya kuhusu ishu hiyo akisema hajafanya jambo hilo kwani ni mchezaji anayejielewa.
Ipo hivi. Yanga inatajwa kama klabu ya kwanza kuzungumza na mchezaji huyo kwa lengo la kutaka kumsajili kabla ya Simba haijaingilia dili hilo kwa kumalizana na mabosi wa Singida Fountain Gate na kutoa baraka zote kwa mchezaji huyo kuchagua mahali anapotaka kwenda.
Mwanaspoti liliripoti mapema kwamba huenda staa huyo akasaini mkataba kujiunga na Yanga ili kwenda kumsaidia Khalid Aucho lakini mambo yakaenda tofauti baada ya Simba kuingilia dili hilo na kumnasa kiungo wa zamani wa Geita Gold.
Mara baada ya Mwanaspoti kuweka bayana juu ya ishu ya Kagoma kutakiwa na Simba, kuliibuka sintofahamu na mijadala ya kimichezo mtandaoni na hata kwa baadhi ya redio kwamba kiungo huyo amesaini klabu mbili na yupo katika hatari ya kufungiwa iwapo suluhu haitapatikana mapema.
Hata hivyo, Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na kiungo huyo na kusema hajasaini mara mbili kama inavyodaiwa na kwamba wanaovumisha ni midomo yao na hana uwezo wa kuwazuia kuzungumza, ila ukweli anaujua yeye.
“Hao wanaoandika mitandaoni kunihusu mimi hawajui wanachokifanya, kila mtu anaandika anachokitaka yeye acha waendelee kufanya hivyo, ukweli naujua mimi na kila kitu kitawekwa wazi mambo yakikamilika,” alisema Kagoma na kuongeza;
“Kila mtu ana uhuru wa kuzungumza anachojisikia kuzungumza siwezi kumzuia mtu, acha waongee ila ukweli wangu naujua mimi na moja ya timu ambayo nimemalizana nayo pia siwezi kusema ni ipi muda ukifika kila kitu kitawekwa wazi.”
Licha ya Kagoma kuficha timu aliyomalizana nayo, lakini rafiki wa karibu wa mchezaji huyo amelidokeza Mwanaspoti kwamba amesaini mkataba wa miaka miwili na Simba na muda wowote klabu hiyo itamtambulisha.
“Kagoma ameshamalizana na Simba, tayari klabu hiyo imemsainisha kiungo huyo mkataba wa miaka miwili kwa thamani kubwa zaidi ya ofa waliyotuma mabosi wa Yanga ili kumng’oa kiungo huyo ambaye alikuwa bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Singida,” kilisema chanzo hicho na kudokeza ishu za madai amesaini mara mbili alisema sio za kweli kwani Yanga ilizungumza naye tu na haikumpa fedha wala mkataba.
Mwanaspoti lilimsaka Rais wa Singida FG, Japhet Makau ili kujua ukweli ulivyo juu ya klabu ipi iliyomalizana na mchezaji huyo naye alisema, muda ukifika kila kitu kitawekwa wazi na wao wametoa baraka zote kwa mchezaji endapo ofa yao itakamilika.
“Kagoma alikuwa nje ya timu kwa muda kwa ruhusa maalumu na kuhusiana na mpango wa kuondoka ndani ya timu kwetu tumetoa baraka zote, lakini hilo litatimia baada ya ofa alizonazo tukishaenda nazo sawa kila kitu kitawekwa wazi,” alisema.