Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagoma aichagua Simba, aitosa Yanga

Yusuph Kagoma Ajiondoa Singida, Anukia Yanga.jpeg Kiungo mkabaji wa Singida Fountain Gate, Yusuph Kagoma.

Mon, 3 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ikiwa imedhamiria kuboresha kikosi chake kuelekea msimu mpya wa mashindano, Simba inatajwa imekaribia kumnasa kiungo mkabaji wa Singida Fountain Gate, Yusuph Kagoma, ambaye awali alitajwa yuko kwenye rada za mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga.

Habari kutoka ndani ya Singida Fountain Gate zinasema, Simba imeingia kati dili hilo, huku mchezaji mwenyewe pia akionekana kufurahia kujiunga na Wekundu wa Msimbazi ambako anaona ni rahisi zaidi kupata namba kwa sasa kuliko akitua Jangwani.

"Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza, ilileta ofa mambo yakawa mazuri na hata sisi tulijua anakwenda huko, ghafla upepo umebadilika, Simba wameingilia kati, ingawa ofa yao si kubwa sana, lakini mchezaji mwenyewe ameonyesha anapenda kwenda huko. Katuambia mwenyewe akienda Msimbazi ana uhakika moja kwa moja na namba," kilisema chanzo chetu.

Kiliongeza katika mazungumzo yao, Kagoma amewaambia endapo akienda Yanga kutakuwa na changamoto kidogo kwa sababu namba anayocheza yupo, Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Jonas Mkude na Zawadi Mauya, hivyo kutakuwa na vita ya kupata nafasi ya kucheza ukilinganisha na Simba.

"Ndugu yangu mwandishi, Kagoma ni kiungo mkabaji mzuri sana, anakaba vizuri, hana rafu za ajabu ajabu kama walivyo viungo wengi wa aina hiyo, na Simba inakosa mtu mkabaji halisi pale kati kwa muda mrefu, yeye anajua hilo, anaona ni fursa ya kwenda kuingia moja kwa moja kwenye kikosi.

Pale kina Babacar Sarr, Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin, hawawezi kumweka nje kwa sababu kama unalijua soka na unaangalia Simba wanavyocheza, wale siyo namba sita, ni nane, wanalazimika kwa sababu hakuna mwenye namba halisi," kilisema chanzo hicho ndani ya Singida Fountain Gate.

Kama Simba itafanikiwa kumalizana na mchezaji huyo, atakuwa wa pili kwa wachezaji wa ndani, baada ya kuwapo kwa taarifa za kumnasa beki wa kati ya Coastal Union, Lameck Lawi.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kwa sasa wana watu ambao wametapakaa kila eneo la Afrika kusaka wachezaji bora, lakini pia wanaangalia wachezaji wa ndani wenye hadhi ya kuichezea timu hiyo ambao walifanya vyema katika Ligi Kuu msimu uliomalizika.

"Tumeshasema tutafanya usajili mkubwa mno, ila kwa sasa hatuwezi kuwataja ni nani atasajiliwa na nani ataachwa, mpaka pale muda wa kufanya hivyo utakapofika," Ahmed alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live