Kiungo wa Singida Big Stars, Yusuph Kagoma ametaja siri ya kuonesha kiwango kikubwa na kumshawishi kocha wa timu hiyo Hans Van Pluijm kumwanzisha katika kikosi cha kwanza.
Kagoma ambaye amesajiliwa dirisha dogo la usajili akitokea Geita Gold ameonesha uwezo mkubwa katika michezo ya Ligi Kuu Bara na katika mashindano ya Mapinduzi Cup yaliyomalizika hivi karibuni visiwani Zanzibar.
Kiungo huyo amekuwa akianza katika nafasi ya kiungo pamoja na Said Ndemla na Bruno Gomez kwenye kikosi hicho ambacho kinashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kikiwa na pointi 43, baada ya ushindi dhidi ya Azam FC juzi kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida.
Kagoma alisema siri kubwa ya mafanikio yake ni kujituma kufuata maelekezo ya kocha pamoja na kucheza kwa kuipambania timu.
“Niwaombe mashabiki waendelee kutupa ushirikiano sisi hatutawaangusha na mchango wao katika timu ni mkubwa na tunauhitaji,” alisema.
Kuhusu mchezo dhidi ya Azam uliomalizika kwa Singida Big Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 alisema walicheza vizuri licha ya Azam kucheza kwa kuwapania kutokana na kuwafunga katika michuano ya Mapinduzi Cup.
Katika michuano ya Mapinduzi, Singida Big Stars iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali, uliofanyika visiwani Zanzibar.
Sambamba na Ndemla, Bruno na Kagoma, Singida Big Stars ina kiungo mwingine matata aliyetua dirisha dogo la usajili wa Januari mwaka huu, Kelvin Nashon.