Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere kushusha presha mashabiki wa Simba

32952 PIC+NKANA

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

SIMBA inacheza na Nkana Red Devils kesho Jumapili Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, wataalamu wa soka nchini, wamemtaja Meddie Kagere kwamba ndiye atakayeipa ushindi timu hiyo kutokana na aina ya uchezaji wake.

Mbali na hilo pia wamewataka mastaa wa Simba kuongeza umakini wa hali ya juu na kuepuka kufanya makosa kama wanayoyafanya kwenye Ligi Kuu Bara.

Mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay aliwapa mbinu Simba ya kushinda mechi ya marudiano na Nkana Red Devils kwamba wawakabe kuanzia juu na wasiruhusu mipira ifike mpaka kwenye ngome yao ya ulinzi inayoongozwa na Pascal Wawa.

"Simba ilifungwa na Nkana mabao 2-1 kutokana na kuwaruhusu wachezee mpira dakika 45 za mwanzo walizozitumia washambuliaji wao hatari Ronald Kampamba na Walter Bwalya, kipindi cha juu walifanikiwa kupunguza mashambulizi baada ya kocha Patrick Aussems kuaambia waanze kukabia juu.

"Pascal Wawa hakuwa na makosa ya moja kwa moja katika mechi hiyo kwani yeye ni mtu wa mwisho kuna watu walizembea majukumu yao kuruhusu mipira kumfikia ni kweli hana kasi ila ana maarifa,"alisema.

KIKOSI CHA KUANZA

Mayay alishauri safu ya ushambuliaji ya Simba katika mechi na Nkana Red Devils, aanze Medddie Kagere, kocha Aussems ataamua ampange na Emmanuel Okwi ama John Bocco ambao aliwataka wasitafute mipira kazi yao iwe kusimama mbele kuhakikisha wanazitumia vyema nafasi za kufunga.

Viungo ni Chama, Dilunga, Kotei na Mkude

Katika safu ya kiungo Mayay, alisema Clatous Chama na Hassan Dirunga wacheze juu kutokana na uwezo wao wa kupushi mashambulizi na wana uwezo wa kufunga na James Kotei acheze kiungo ya chini asaidiane na mabeki kukaba huku mbadala wake akimtaja kuwa ni Jonas Mkude.

Mabeki ni Wawa, Nyoni, Kwasi na Gyan

Kwa upande wa mabeki Mayay alisema bado anamuona Wawa kuwa kiongozi wa wenzake akitaka acheze na Erasto Nyoni, lakini beki wa kushoto awe Asante Kwasi akionyesha kutomwamini Mohamed Hussein 'Tshabalala' huku beki wa kulia akimtaka acheze Nicholas Gyan licha ya kukiri kwamba hawezi kuziba pengo la Shomary Kapombe ambaye anauguza majeraha.

Winga Kichuya na kipa Manula

"Shiza Kichuya ni winga ambaye yupo vizuri anaweza akakisaidia kikosi hicho, ingawa akipata matatizo wanaweza wakamchezesha Said Ndemla ambaye ameonyesha uwezo katika mechi na KMC, lakini kipa bado anastahili kucheza Aishi Manula licha ya kuwa na makosa yanayojirudia ya kufungwa mipira ya mbali,"alisema.

Nyota ambao aliwaona wameonyesha uwezo Simba walipocheza na KMC aliwataja kuwa ni Adam Salamba aliyemuelezea kuwa bao alilofunga haikuwa nafasi bali alijiongeza na kuonyesha yeye ni fundi wa kumalizia.

Wengine aliowataja ni Mzamiru Yasin kwamba aliichezesha timu kwa umakini wa hali ya juu na kutoa pasi ya Said Ndemla "Ndemla, Mzamiru, Salamba walionyesha kiwango kizuri ila wengine walikuwa wazuri dakika 45 za mwanzo kipindi cha pili walikata pumzi,"alisema.

Naye kocha Kenny Mwaisabula, alisema ili Simba wawafunge Nkana watatakiwa kuingia uwanjani kama wamefungwa na sio kusaka ushindi wa bao moja "Nkana ina washambuliaji wawili ambao ni hatari Kampamba na Bwalya, lazima wawachunge na wawe na kiu ya kufunga mabao mengi,"alisema.

Lakini kikosi alichokiona kinastahili kuanza ni Aishi Manula (kipa) akisema Deo Munishi 'Dida' bado hana umakini na mechi, beki wa kati awe Juuko Murshid na Wawa, Nyoni acheze kulia, upande wa viungo wawe watano Mkude,  Kotei, Chama, Dirunga na Okwi.

Safu ya ushambuliaji alimtaka Aussems amuanzishe Kagere na Bocco "Binafsi naona akiwapanga hivyo wanaweza wakashinda mechi hiyo, ila kikubwa wajitume akili na nguvu zao zifanye kitu ndani ya dakika 90,"alisema.

Kwa upande wa wachezaji ambao walicheza na KMC ambao wanaweza wakawaingiza ndani ya kikosi hicho alisema ni Juuko Murshid, Mzamiru Yasin na Said Ndemla.

NIYONZIMA AWEKWA KANDO

Kocha Mshindo Msolla amemwambia Aussems kwamba ili asonge mbele basi mfumo unaomfaa ni 4-4-2 na kutumia vizuri kikosi chake kipana chenye wachezaji wazuri ambao miongoni mwao walicheza mechi ya ligi dhidi ya KMC na kushinda bao 2-1.

Dr Msolla alisema; "Kagere kwenye mechi hiyo ni lazima aanze, halafu mmoja wao kati ya Bocco na Okwi aanzie pembeni kwani mechi iliyopita haikuwa na mawinga zaidi ya kujaza viungo ambao wote wanacheza kwa mfumo mmoja.

"Aussems aingie uwanjani akiwa amesahau bao la ugenini, Nkana ni timu nzuri na ni lazima wamewasoma hata mechi ya ligi ingawa ujanja aliotumia kocha wa Simba wa kuchezesha wachezaji asiowatumia mara nyingi unaweza kumsaidia kama tu atazingatia kubadili mfumo wake alioutumia Zambia.

"Mimi ni muumizi wa nidhamu, mchezaji kama Juuko Murshid, alicheza vizuri mechi na KMC na hata akipewa mechi na Nkana atafanya vizuri lakini tatizo lake ni nidhamu mbovu aliyonayo, Niyonzima kwangu ni chaguo la tatu huwezi kumuweka nje Clatus Chama au Hassan Dilunga halafu ukamwanzisha Niyonzima.

"Uzuri wa Niyonzima ni mmoja ambapo ni kiungo mkatabaji na hashambulii zaidi ya kupiga pasi za kushoto, kulia na mipira yake ya kurudisha kwa visigino na sio kupeleka mashambulizi, kikubwa kocha aangalie tu nani atampa matokeo mazuri kulingana na upana wa kikosi chake.

"Watu wengi hawafahamu pengine, kwamba kikosi cha kucheza siku ya mechi kinapangwa kulingana na jinsi mchezaji alivyofanya vizuri mazoezini na sio kwenye mechi moja, hivyo mchezaji anaweza kucheza vizuri mechi na KMC ukampa nafasi mechi na Nkana akaharibu zaidi," alisema Dr Msolla

Niyonzima kwa mechi za hivi karibuni hawezi kuwaweka benchi viungo wanaoanzishwa kwenye kikosi cha kwanza.

"Kwa uzito wa mechi hiyo Niyonzima hastahili kuanza kwenye kikosi cha kwanza bado anahitaji apate mechi nyingi za kumrudisha mchezoni, Simba inahitaji kushinda inatakiwa iwapange wenye viwango vya juu,"alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz