Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere kuikosa Singida, Nsajigwa amhofia Julio

Kagere Mk 14 Kagere kuikosa Singida, Nsajigwa amhofia Julio

Fri, 15 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha msaidizi wa Namungo, Shadrack Nsajigwa amesema mabadiliko ya benchi la ufundi la Singida Fountain Gate kwa kumleta kocha mpya, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ yataleta ugumu katika mchezo wa kesho kwani yatabadilisha upepo kwenye kikosi cha Walima Alizeti hao.

Julio ameteuliwa mapema wiki hii kuwa kocha mkuu wa Singida akisaidiwa na Ngawina Ngawina na Ally Mustapha ‘Barthez’ wakichukua mikoba ya Thabo Senong na Nizar Khalfani.

Namungo itakuwa ugenini kesho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa kuvaana na Singida Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu ambao Nsajigwa amekiri utakuwa mgumu, lakini ametamba wamejiandaa vyema kuhimili presha hiyo.

Nsajigwa amesema timu inapofanya mabadiliko ya benchi la ufundi wachezaji huwa wanapata morali, hata hivyo akawatoa wasiwasi mashabiki wa Namungo, wamefanya maandalizi mazuri ya kupata ushindi.

“Hilo halitupi shida, tumeshajiandaa kushindana nao, tunajua nini ambacho wanakifanya, uwezo wao tunaheshimu na wana upungufu yapi, kwa hiyo tumejiandaa kwenye sehemu hizo kwa ajili ya kushindana nao ili kesho tupate ushindi,” amesema Nsajigwa.

“Tumefika juzi, maandalizi yetu yanakwenda vizuri na hadi sasa tunajua mchezo utakuwa mgumu kutokana na nafasi tuliyopo kwenye ligi na wapinzani wetu hawajapata ushindi kwa muda mrefu na wamefanya mabadiliko ya makocha.”

Kocha huyo amesema katika mtanange huo watamkosa mshambuliaji wao, Meddie Kagere ambaye masharti yanamzuia kucheza kwani amejiunga dirisha dogo akitokea Singida, huku nyota wengine watakaokosekana ni Kelvin Sabato na Frank Domayo mwenye matatizo ya kifamilia.

“Bado malengo yetu ni kumaliza katika nafasi nne za juu na ukiangalia pointi zetu hatuko mbali kwa sababu aliye nafasi ya nne ana alama 30, tuna tofauti ya pointi saba na tumebakiza michezo 10, kwa hiyo lolote linaweza kutokea,” amesema.

Mchezaji wa timu hiyo, Ayoub Semtawa amesema benchi la ufundi limewapa mbinu nzuri kwa mchezo wa kesho na wachezaji wako tayari kwenda kuzifanyia kazi nzuri leo.

“Wapinzani wetu wanacheza vizuri japokuwa hawapati ushindi, hivyo tunakwenda kuwakabili kama wapinzani walio bora na tuna imani tutapata ushindi, kwa hiyo tumejiandaa vizuri kuwakabili,” amesema.

Chanzo: Mwanaspoti