Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere atupia mbili, Simba yaichakaza JKT Tanzania

Thu, 29 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mfungaji bora wa msimu uliopita Meddie Kagere amefunga mabao mawili akiwaongoza mabingwa watetezi Simba kuichapa JKT Tanzania mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kagere msimu uliopita aliweka rekodi ya kufunga mabao 23, ameanza msimu kwa kishindo akifunga mabao yake mawili katika dakika ya 2 na 58 kabla ya kutegeneza bao la tatu la Simba lililofungwa na Miraj Athumani katika dakika ya 73, huku Edward Songo akifunga bao la kufutia machozi kwa JKT Tanzania katika dakika 87.

Ushindi huo wa Simba unawaweka kileleni kwa Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya mabao na kuwafuta machungu mashabiki wake ambao mwishoni mwa wiki walishuhudia mabingwa hao wakitolewa katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa na UD Songo ya Msumbiji baada ya kulazimishwa sare 1-1 nyumbani.

Simba ilianza mchezo huo kwa kasi na dakika ya pili Kagere alifunga bao kwanza akimalizia vizuri pasi ya kiungo Clatous Chama.

Baada ya Simba kupata bao hilo walitulia na kumiliki mpira muda mwingi huku wakitengeneza nafasi za kufunga.

Nafasi hizo za kufunga walikutana nazo Chama, Deo Kanda, Tairone Zaguiero na Gerson Fraga ambao kama wangekuwa makini walikuwa na uwezo wa kuongeza bao.

Pia Soma

JKT Tanzania wenyewe walikuwa wakifanya mashambulizi ya kushtukiza pamoja na kucheza mchezo wa kutumia nguvu zaidi jambo lililofanya wachezaji wake wawili kupewa kadi za njano.

Eneo la katikati ya uwanja viungo wa JKT, Jabir Aziz na Mwinyi Kazimoto walionekana kupashika na kumiliki mpira dhidi ya wenzao wa Simba.

Wachezaji wawili Wabrazili wa Simba, Tairone Zaguiero aliyecheza beki wa kati na Gerson Fraga aliyecheza kiungo mkabaji walionekana kuanza vizuri.

Zaguiero alicheza kwa maelewana na Erasto Nyoni huku wakifanikiwa kuwazuia washambuliaji wa JKT Tanzania Hassan Mwatelemwa na Daniel Lyanga kutokufunga bao.

Zaguiero alikuwa mzuri pia katika kushambulia kwani alianzisha mashambulizi na hata muda mwingine kwenda kupiga mipira ya vichwa anayotokana na kona au faulo.

Kuanza kwake katika kikosi cha kwanza Zaguiero kumetokana na kuumia kwa beki Pascal Wawa.

Fraga alikuwa akitimiza jukumu lake la kukaba kama kiungo mkabaji huku akipora mipira mingi kwa viungo wa JKT kama Mwinyi Kazimoto na Jabir Aziz.

Simba sasa inakwenda kwenye mapumziko ya wiki mbili kupisha mechi za timu za taifa ikiwa kileleni huku watani zake Yanga wakiwa miongoni mwa timu za mkiani.

Chanzo: mwananchi.co.tz