Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere atuma salamu Simba

Meddie Kagere Mk14 Meddie Kagere

Wed, 9 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Singida Big Stars leo Jumatano itakuwa nyumbani Uwanja wa Liti dhidi ya Simba mechi ya Ligi Kuu itakayokuwa na ushindani mkali lakini kubwa zaidi ni nyota wa SBS, Meddie Kagere kuwatumia salamu mabosi wake wa zamani.

Mbali na Kagere, Simba itakutana na mastaa wake wa zamani kina Pascal Wawa, Said Ndemla, Nicolas Gyan na Amissi Tambwe ambao wameapa kubakiza pointi tatu nyumbani.

Kagere ameanza kuonyesha makali yake ya kufunga bao lake la kwanza kwenye Ligi Kuu, juzi Jumapili dhidi ya Polisi Tanzania na kuiwezesha Singida kushinda 1-0 ugenini.

Kagere aliyeichezea Simba misimu minne tangu mwaka 2018 alipojiunga nayo akitokea Gor Mahia ya Kenya akiipa makombe matatu ya ligi mfululizo na kuibuka mfungaji bora misimu yake miwili ya mwanzo alijiunga Singida mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuachana na Simba na kesho kwa mara ya kwanza atakutana na waajili wake hao wa zamani na ametamba kutowaonea huruma.

Nyota huyo kutoka Rwanda alisema kazi yake ni kuipambania timu yake kupata ushindi na kufikia malengo hivyo kama atapata nafasi ya kufunga atafanya hivyo kama ilivyo kawaida yake.

“Simba tulimalizana, kwa sasa nipo Singida kutimiza malengo ya timu hivyo nitajitahidi kutumia kila nafasi nitakayoipata ili kupata ushindi na kutimiza malengo yake,” alisema Kagere aliyemaliza msimu uliopita akiwa na mabao saba ndani ya Simba.

“Nimefurahi kuanza kufunga, ni jambo nililokuwa natamani kufanya kwa muda mrefu tangu nimetua hapa na naamini huo ni mwanzo tu, nitafanya vizuri zaidi kwenye mechi zijazo.” alisema.

Kwa upande wa Ndemla alisema mechi itakuwa ngumu kwa pande zote mbili;

“Kwetu ushindi ni jambo muhimu hilo linawezekana kwani wachezaji baada ya mechi na Polisi Tanzania tulikubaliana kuifunga Simba kwenye uwanja wetu wa nyumbani,” alisema Ndemla na kuongeza;

“Mechi kubwa kama hizi zinazokutanisha wachezaji wakubwa waliocheza pamoja kwa nyakati tofauti huwa zinaamuliwa na vitu viwili mbinu za timu pamoja na ubora wa mchezaji mmoja mmoja.”

Naye Wawa alisema Singida ina wachezaji wengi wazuri wenye sifa za kucheza Simba, Yanga na Azam kwa maana hiyo haitakuwa rahisi kwa upande wao kukubali kupoteza.

“Mchezo utakuwa mgumu binafsi wenye mbinu nyingi kwa kila timu na kwetu tunahitaji pointi tatu kwani zitatuweka kwenye mazingira mazuri katika ligi msimu huu,” alisema Wawa.

Singida, Azam na Simba zinalingana alama (17), Simba inashika nafasi ya pili baada ya kucheza mechi nane na kufunga jumla ya mabao 17 wakifungwa manne jambo linaloifanya kuwa juu ya Singida na Azam kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na mbili hizo zimecheza mechi tisa kila moja.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Singida (Sirefa) Juma Mwendwa alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na viingilio jukwaa kuu VIP itakuwa Sh 10,000 na mzunguko Sh 5000 ambapo zitaanza kuuzwa leo jirani na uwanja na eneo la Stand na soko kuu la Singida.

Chanzo: Mwanaspoti