Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere atuliza maumivu Simba

73531 Simba+pic

Fri, 30 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Simba imewapoza machungu mashabiki wake, baada ya jana kuanza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kishindo kwa kuichapa JKT Tanzania mabao 3-1.

Mshambuliaji Meddie Kagere alifunga mabao mawili katika mchezo huo na jingine likifungwa na Miraji Athumani. Mchezo huo ulichezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kagere alifunga mabao hayo dakika ya kwanza kwa kiki baada ya kupata pasi ya Clatous Chama kabla ya Miraji kuongeza la pili dakika ya 73 kwa kichwa akipata pasi ya Kagere.

Mchezaji huyo raia wa Rwanda, ameanza kwa kasi mbio ya kuwania kiatu cha dhahabu kama ilivyokuwa msimu uliopita ambao aliibuka mfungaji bora akifunga mabao 23.

Mshambuliaji Salim Aiyee aliyekuwa Mwadui (sasa KMC) alishika nafasi ya pili kwa mabao 18 akifuatiwa na Heritier Makambo aliyekuwa Yanga aliyefunga 17.

Bao la JKT Tanzania lilifungwa dakika ya 87 na Edward Songo kwa kiki kali ya mbali ya mguu wa kulia baada ya kumpima kipa Aishi Manula aliyekuwa amesogea kidogo mbele ya lango.

Pia Soma

Advertisement   ?
Mashabiki wa Simba wametuliza machungu ya timu yao kuondoshwa mapema katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya UD Songo ya Msumbiji, Jumapili iliyopita.

Tangu Simba ilipoondoshwa katika mashindano hayo, idadi kubwa ya mashabiki wake walikuwa wanyonge kabla ya jana kuzinduka kufuatia ushindi huo mnono.

Kocha Patrick Aussems alibadili kikosi kama alivyoahidi siku moja kabla ya mchezo, baada ya kuwatumia Wabrazili wawili beki Tairone Zaguiero na kiungo Gerson Fraga.

Pia alimpanga kiungo Mzamiru Yassin na alimuanzisha Hassani Dilunga ambaye mara nyingi amekuwa akitokea benchi.

“Matokeo ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika yalituathiri kwa namna moja au nyingine ndio maana nimefanya mabadiliko ya kikosi jambo ambalo huwa sipendi kufanya mara kwa mara,” alisema Aussems.

Pia alisema anafurahishwa na kazi nzuri ya Kagere anayofanya katika mechi za Simba na amemtaja ni mshambuliaji hodari mwenye uwezo wa kujiweka vyema katika nafasi. Pamoja na ushindi huo, Simba haikucheza kwa kiwango bora katika eneo la kiungo kwani Mzamiru alipoteza pasi mara kwa mara, lakini Fraga hakuwa na kasi ya kutosha.

Mzamiru na Fraga walipata kazi kupenyeza mipira mbele kwa akina Kagere kwa kuwa JKT Tanzania iliingia na mfumo wa kujaza idadi kubwa wachezaji wa kiungo.

Kiungo Mohammed Fakhi mara kadhaa alikuwa akitibua mipango ya Mzamiru na Fraga. Mfumo huo uliilazimisha Simba kucheza pasi za nyuma kwa mabeki wa kati Erasto Nyoni na Tairone ili kuanzisha mashambulizi.

Kocha wa JKT Tanzania Yohana Challe, alisema pamoja na kutumia mfumo huo, lakini walifanya makosa ambayo yameigharimu timu yake katika mchezo huo.

“Tumefanya makosa na wenzetu wametuadhibu, tunajipanga kwa mechi ijayo,”alisema Challe.

Dakika ya 77 Ibrahim Ajibu aliibua shangwe kwa mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuingia kwenda kujaza nafasi ya Chama.

JKT Tanzania: Abdulrahman Mohammed, Madenge Ramadhani, Edward Charles, Mohammed Fakhi, Rahim Juma, Jabir Azizi, Mwinyi Kazimoto, Hafidh Mussa, Hassani Matalema, Daniel Lyanga na Ally Bilali.

Simba: Aishi Manula, Haruna Shamte, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Tairone Santos, Gerson Fraga, Deo Kanda, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Hassani Dilunga na Clatous Chama.

Chanzo: mwananchi.co.tz