Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere apewa mbinu kuiua Simba

Meddie Kagere Singida Meddie Kagere

Fri, 3 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Benchi la ufundi la Singida Big Stars limempa Meddie Kagere kazi maalumu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kesho dhidi ya Simba katika Uwanja wa Mkapa.

Kagere katika michezo mitano iliyopita ya ligi ameanza michezo miwili, akitokea kwenye benchi miwili huku akikosekana katika mchezi dhidi ya Geita Gold.

Hata hivyo, mchezo uliopita wa Kombe la Azam (ASFC) dhidi ya Ruvu Shooting alikuwa kwenye kikosi cha kwanza na kutupia mabao mawili katika ushindi wa mabao 2-0 akiivusha timu hiyo hadi hatua ya 16 bora.

Kocha msaidizi wa Singida, Mathias Lule alisema kukosekana au kuanzia benchi katika michezo hiyo ni moja ya mbinu ambazo benchi la ufundi lilikuwa linafanya kutokana na wapinzani wao walivyo.

“Unapokabiliana na timu yoyote lazima ujue mazuri yake na udhaifu wake, hivyo unapokuwa na mchezaji aina ya Kagere inakupa upana wa kumuanzisha au kumwacha kwanza nje.

“Tunakutana na Simba ambayo aliwahi kucheza kwa misimu kadhaa, hivyo sio Kagere pekee yake bali kila mmoja anajua kitu gani tunakihitaji na anapaswa kufanya nini,” alisema Lule.

Aliongeza kuwa wamesafiri na kikosi kizima na hakuna mchezaji ambaye ana tatizo kiafya, hivyo wana imani kila atakayepata nafasi ya kuanza atafanya vyema.

Kagere mwenye mabao matano msimu huu, alijiunga na Simba msimu wa mwaka 2018/19 akitokea Gor Mahia ya Kenya na kuitumikia timu hiyo kwa misimu minne mfululizo akifunga mabao 65 kwenye ligi.

Nyota huyo akiwa Simba aliibuka mfungaji bora wa msimu wa Ligi Kuu mara mbili - msimu wa 2018/19 akifunga mabao 23 na 2019/20 akitupia kambani mabao 22 ilhali msimu wa 2020/21 mabao 13 na uliopit mabao saba.

Singida katika michezo 10 ya ugenini msimu huu imepoteza mitatu dhidi ya Yanga ikilala kwa mabao 4-1 huku Fiston Mayele akitupia matatu ‘hat trick’, ikapoteza 1-0 mbele ya Mtibwa na mara ya mwisho kufungwa ugenini ilikuwa Oktoba 3 dhidi ya Azam ilipopigwa bao 1-0.

Chanzo: Mwanaspoti