Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagere, Bocco ‘waharibu’ kibarua cha Pluijm Azam

43560 Pic+bocco Kagere, Bocco ‘waharibu’ kibarua cha Pluijm Azam

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kibarua cha kocha wa Azam, Hans van der Pluijm ambaye ni raia wa Uholanzi kimeota nyasi baada ya jana kutimuliwa ikiwa ni siku moja tangu akutane na kipigo juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba.

Mabao ya Meddie Kagere aliyofunga mara mbili na lile la John Bocco yalitosha kuizamisha Azam kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Huo ulikuwa mchezo wa tatu wa timu hiyo kupoteza, ilifungwa na Mtibwa Sugar mabao 2-0, Prisons ikashinda bao 1-0 kabla ya kupigwa mabao 3-1 na Simba.

Mabao hayo yanaingia kutengeneza mwenendo mbaya wa timu hiyo ulioonekana wa kusuasua kwani katika mechi tano za mwisho imetoka sare tatu na kupoteza mbili.

Pluijm aliyechukuliwa kutoka Singida United, alitimuliwa baada ya kufanyika kikao kizito cha vigogo wa timu hiyo tangu juzi usiku baada ya mchezo wa Simba.

Mwananchi liliwatafuta viongozi wa timu hiyo akiwemo Mkurugenzi wa timu, Nassor Idrisa na baadaye mwenyekiti wa timu, Abdulkarim Mohamed kuzunguzia hatua hiyo, lakini hata hivyo simu zao hazikuwa na majibu.

Akizungumza na Mwananchi jana, Pluijm mwenyewe alikiri kutupiwa virago na kwamba alikuwa akijiandaa kuanza maisha mapya sehemu nyingine.

“Namtakiwa kocha ajaye mafanikio mema nimekuwa na wakati mzuri hapa na nilijitahidi kadri niwezavyo ili kufikia malengo ya klabu, ninaamini atakayekuja ataendeleza kile nilichofanya.

“Ninawatakiwa mafanikio mema kwa siku chache za usoni na ninaamini Azam wanaweza kutawala soka la Tanzania maana wamejipambanua kwa kuwa na miundo mbinu mingi ya kisasa,” alisema kocha huyo.

Akaongeza; “Asanteni mashabiki wa Azam ambao siku zote hata kwenye kipindi kigumu mlikuwa nyuma yangu mkinisapoti.”

Mholanzi huyo ametimuliwa sambamba na msaidizi wake Juma Mwambusi ambaye alijiunga naye Azam mara baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja akitokea Singida United. Wote kwa pamoja waliwahi kuhudumu Yanga kwa mafanikio.

Kocha wa KMC, Etienne Ndayiragije ambaye ameifanya timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni kuwa moja ya timu tishio Ligi Kuu anatajwa kuwa huenda akachukua mikoba akishirikiana na mmoja wa makocha wasaidizi, Iddi Cheche .



Chanzo: mwananchi.co.tz