Mchezo wa raundi ya tano Ligi Kuu Bara kati ya KMC na Kagera Sugar umemalizika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa wenyeji KMC kupoteza nyumbani kwa kufungwa bao 1-0.
Mechi ilianza kwa timu zote kushambuliana kwa kupokezana lakini Kagera ndio walionekana kuwa bora zaidi katika dakika 20 za mwanzo.
Dakika ya 16, Meshack Abraham aliipatia bao la kongoza Kagera lililodumu hadi dakika 45 za kwanza akifunga kwa kona baada ya kutokea kona tatu mfululizo langoni kwa KMC.
KMC walionesha nia ya kutaka kusawazisha bao hilo kwa kuwatumia viungo Awesu Awesu, Miraji Athuman na mabeki Nickson Kibabage na Kelvin Kijiri lakini jitihada zao zilikwamia kwenye ngome ya Kagera ikiongozwa na Steven Duah na Abdallah Mfuko.
Timu zote ziliendelea kufanya mabadiliko, KMC ikimtoa Matheo Antony dakika ya 53 na kuingi Abdul Hillary huku Kagera ikiwatoa Meshack na Erick Mwijage dakika ya 60 na nafasi zao kuchukuliwa na Peter Mwalyanzi na Jackson Kibirige na dakika mbili baadae KMC ilimtoa Charles Ilamfya na kuingia Hassan Kabunda.
Mabadiliko hayo yalionekana kuongeza nguvu kwa timu zote mbili na dakika ya 59 Kagera kupitia kwa Hassan Mwaterema ilikosa bao la wazi akibaki yeye na kipa na KMC kukosa bao dakika ya 62 kupitia kwa Kenny Ally.
KMC iliendelea kutafuta bao la kusawazisha na dakika ya 70 ilifanya mabadiliko mengine kwa kuwatoa Awesu na Miraji ambao nafasi zao zilichukuliwa na Mohamed Samatta na Idd Kipagwile.
Dakika ya 79 Hilarry wa KMC alioneshwa kadi ya njano baada ya kumchezea faulo mchezaji wa Kagera ikiwa ni kadi ya pili katika mchezo huo baada ya ile ya Kibabage aliyoipata katika kipindi cha kwanza.
Kagera Sugar dakika ya 83 ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Mbaraka Yusuph na Nassor Kapama na nafasi zao kuchukuliwa na David Luhende na Abdallah Seseme walioingia kuongeza umiliki wa mpira kwa Kagera.
Dakka ya 90 Kagera ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Mwaterema na nafasi yake kuchukuliwa na Ally Rucha na dakika hiyo hiyo kipa wa Kagera Ramadhan Chalamanda alioneshwa kadi ya njano baada ya kumdanganya mwamuzi.
Ushindi huo unaifanya Kagera kupanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi baada ya kufikisha alama nane ikiwa imecheza mechi nne huku KMC ikisalia nafasi ya 15 na alama zake mbili baada ya mechi tano.