Benchi la Ufundi la Kagera Sugar limesisitiza ushindi kuelekea mchezo wa Hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Mbeya City.
Mchezo huo utapigwa leo Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, huku miamba hiyo ikifanya maandalizi ya mwisho jana Jumamosi (Machi 04) mjini Bukoba.
Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar Marwa Chamberi amesema lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo na kutinga Robo Fainali, ndio maana wamefanya maandalizi makubwa ya kuikabili Mbeya City.
“Ushindani ni mkubwa na kila timu inapambana kufanya vizuri, ambacho tunakihitaji sisi katika mchezo wetu wa kesho ni kushinda na uwezo huo tunao baada ya kufanya maandalizi ya kutosha.”
“Tunaiheshimu sana Mbeya City kwa sababu ni timu ambayo ipo katika hadhi ya Ligi Kuu, na hilo ndilo linatuaminisha mchezo utakua mgumu, lakini imani kubwa zaidi tulionayo ni kusaka matokeo ndani ya dakika 90 katika Uwanja wetu wa nyumbani.”
“Hadi sasa wachezaji wetu wote wapo vizuri na wanapambana kupata matokeo, tuna imani kubwa watatupa matokeo mazuri kama walivyotuonesha kwenye mazoezi yetu.” amesema Chamberi
Michezo mingine ya ASFC Hatua ya 16 Bora imechezwa jana Jumamosi, ambapo Ihefu FC ikiwa nyumbani Highland Estate mkoani Mbeya, kuikaribisha Pan Africans kutoka jijini Dar es salaam, huku Mtibwa Sugar ikiikabili KMC FC ya Dar es salaam katika Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.
Azam FC itakua nyumbani Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam leo Jumapili (Machi 05) kuikabili Mapinduzi FC.
Wakati miamba hiyo ikijiandaa kukutana leo katika Uwanja wa Azam Complex, tayari timu nyingine zimeshafuzu Hatua ya Robo Fainali ya ASFC baada ya kushinda michezo yao wa Hatua ya 16 Bora.
Timu hizo ni Simba SC, Geita Gold FC, Young Africans na Singida Big Stars, Ihefu Mtibwa.