Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagera Sugar yaichapa Mwanza Kombaini 6-0 ikiiandalia dozi Geita Gold

Kagera Sugar X Mwanza Kombain Kikosi cha Kagera Sugar

Sat, 3 Sep 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kukipiga na Geita Gold katika mchezo wa Ligi Kuu Septemba 6, Kagera Sugar imeendelea na maandalizi kuelekea mtanange huo ambapo jana imeibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Mwanza Kombaini.

Mchezo huo wa kirafiki wa kujipima uwezo umepigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza saa 10:18 jioni ambapo Kagera Sugar imeibuka na ushindi huo mnono huku nyota mpya wa kikosi hicho, Yusuph Mhilu aliyerejea kutoka Simba akianza rasmi kuitumikia timu hiyo.

Katika mtanange huo Kagera Sugar ambayo safu yake ya ushambuliaji imeongozwa na Hamis Kiiza, Yusuph Mhilu na Abeid Athuman imetandaza soka safi mbele ya Mwanza Kombaini ambayo haishiriki michuano yoyote.

Kagera Sugar ambayo imeutumia mchezo huo kujipima kwa ajili ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Jumanne ijayo dhidi ya Geita Gold, iliandika bao la kuongoza mnamo dakika ya 12 likifungwa na Abdallah Seseme aliyeichambua ngome ya wapinzani na kupiga shuti lililojaa moja kwa moja nyavuni.

Wana Nkurunkumbi wamepata bao la pili katika dakika ya 29 likifungwa na Abeid Athuman huku bao la tatu likipachikwa na mkongwe, Hamis Kiiza 'Diego' dakika ya 40 na kuipeleka timu hiyo mapumziko ikiwa kifua mbele kwa mabao 3-0.

Kipindi cha pili, Kagera Sugar imeanza kwa mabadiliko ya kipa said Kipao aliyechukua nafasi ya Ramadhan Chalamanda na kuendelea kulisakama lango la Mwanza Kombaini ambapo ilipata bao la nne dakika ya 59 kupitia kwa Meshack Abraham.

Baada ya bao hilo, benchi la ufundi la Kagera Sugar limefanya mabadiliko kwa kuwatoa wachezaji wote walioanza kipindi cha kwanza, mabadiliko hayo yamelipa dakika ya 84 na 90 yakiipa mabao mawili yakifungwa na Abubakar na Kassim Feka ambapo timu hiyo imeibuka na ushindi wa mabao 6-0.

Kocha msaidizi wa Kagera Sugar, Marwa Chambeli amesema mchezo huo ni kipimo kizuri kwani kuna vitu walilenga kuviangalia ikiwemo kufunga mabao na wanategemea kucheza mchezo mwingine wa kirafiki kabla ya kuivaa Geita Gold.

Chanzo: Mwanaspoti