Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagera Sugar, Ruvu Shooting ngoma ngumu dakika 45

Kagera Sugar Vs Ruvu Shooting Kagera Sugar, Ruvu Shooting ngoma ngumu dakika 45

Sat, 15 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Dakika 45 za kipindi cha kwanza mchezo wa Ligi Kuu kati ya Kagera Sugar na Ruvu Shooting zimemalizika huku timu hizo zikitoshana nguvu.

Mchezo huo ambao unapigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza umekwenda mapumziko bila mbabe kupatikana baada ya kufungana bao 1-1.

Mtanange huo ambao timu zote zinacheza kwa kasi, pasi nyingi na kushambuliana kwa zamu huku kukiwa na kosa kosa umekuwa wa burudani kwa mashabiki wachache ambao wamejitokeza uwanjani hapo.

Kagera Sugar ndiyo wamekuwa wa kwanza kupata bao dakika ya tisa likifungwa na mkongwe, Hamis Kiiza ambaye ametuliza krosi safi kutoka kwa Anuary Jabir akageuka na kufumua shuti ambalo limemshinda kipa wa Ruvu Shooting, Hussein Masalanga.

Baada ya kupata bao hilo Kagera Sugar wameendelea kulishambulia lango la wageni wao lakini umakini katika safu ya ushambuliaji umewanyima mabao ikiwemo nafasi muhimu mnamo dakika ya 14, ambapo Anuary Jabir akiwa yeyena kipa akapiga shuti lililokwenda nje ya lango.

Licha ya kutanguliwa, Ruvu Shooting walicheza kwa utulivu mkubwa na kutafuta nafasi ya kusawazisha bao hilo ambapo juhudi zao zimelipa mnamo dakika ya 27 wakipata bao.

Bao hilo limefungwa kwa ufundi na Rashid Juma baada ya kupokea pasi ya Abakasim Suleman na kumchambua kipa na kumalizia kwa shuti dogo ambalo limesindikizwa nyavuni na nahodha wa Kagera Sugar, Abdallah Mfuko aliyekuwa akijaribu kuokoa.

Mtanange huo utaendelea muda mfupi ujao kumalizia dakika 45 za kipindi cha pili kupata mbabe atakayeondoka na ushindi.

Chanzo: Mwanaspoti