Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kagame kuna vita ya ndugu

Kagame Pc Kagame kuna vita ya ndugu

Fri, 12 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya jana kuwa katika mapumziko, michuano ya Kombe la Kagame 2024 inatarajiwa kuendelea leo kwa michezo minne ukiwamo wa wanandugu, Coastal Union na JKU Zanzibar zitakazovaana mapema saa 7:00 mchana kwenye Uwanja wa KMC, jijini Dar es Salaam.

Michuano hiyo iliyoanza Jumanne, inashirikisha timu 12 zilizopangwa katika makundi matatu na mshindi wa kila kundi sambamba na mshindwa bora mmoja zitafuzu nusu fainali itakayopigwa Julai 19 na bingwa mpya anatarajiwa kufahamika baada ya fainali itakayochezwa Julai 21.

Bingwa wa sasa ni Express ya Uganda iliyotwaa taji hilo mwaka 2021 haipo katika michuano ya msimu huu, hivyo taji kuwa halina mwenyewe.

Coastal iliyoanza michuano kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dekadaha ya Somalia itakuwa na kazi ngumu mbele ya mabingwa hao wa Zanzibar walioanza kwa kichapo mbele ya Al Wadi ya Sudan, ambao bila ya shaka itataka ushindi ili kujiweka pazuri.

Wanafainali hao wa mwaka 1989 wanahitaji ushindi kujihakikia nafasi ya kwenda nusu fainali kabla ya mechi ya mwisho dhidi ya Al Wadi, huku kocha mkuu David Ouma akisema anatumia mechi hizo kuliweka vyema jeshi lake kabla ya michuano ya CAF ambayo droo ilifanyika jana alasiri.

Coastal itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa kuanza dhidi  Bravos do Maquis ya Angola na itawakilisha nchi sambamba na Simba na Uhamiaji ya Zanzibar, huku Yanga, Azam na JKU zenyewe zikicheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mbali na mechi hiyo ya wanandugu, leo mashabiki watashuhudia mechi nyingine tatu, ikiwamo ya saa 10 jioni kwenye Uwanja wa KMC kati ya Al Wadi na Dekedaha, huku saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex SC Villa ya Uganda na Singida Black Stars zitakwaruzana, kisha APR na Al Merrikh ya Sudan Kusini zitahitimisha ratiba kwa siku ya leo.

Ratiba: Leo Ijumaa

Coastal v JKU                   (Saa 7:00 mchana)

Al Wadi v Dekadaha        (Saa 10:00 jioni)

SC Villa v Singida BS        (Saa 12:00 jioni)

APR        v Al Merrikh       (Saa 3:00 usiku)

Kesho Jumamosi

Al Hilal   v Red Arrows     (Saa 12:00 jioni)

Gor Mahia v Asas             (Saa 3:00 usiku)

Chanzo: www.tanzaniaweb.live