Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaeda Mzungu wa Yanga mwenye siri nzito

Mzungu Yanga Princess.jpeg Kaeda Mzungu wa Yanga mwenye siri nzito

Mon, 19 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Hivi karibuni timu ya Mwanaspoti ilifunga safari kwenda Mbezi Beach, Dar es Salaam nyumbani kwa wazazi wa kiungo mshambuliaji wa Yanga Princess, Kaeda Wilson ambapo ilikutana na utamaduni tofauti.

Lengo la safari hiyo ilikuwa kufanya mahojiano na Kaeda, mtasha kutoka Marekani, lakini baada ya kufika nyumbani akasalimia na wanahabari wetu na kwenda kuwachukulia maji ya kunywa kisha akawaruka wanaume wawili (miongoni mwa timu hiyo) na kwenda kuwapa wanawake.

Nyota huyo aliyeanza kunonga ndani ya timu hiyo, alirudi tena kuchukua maji mengine glasi mbili, akawapa wanaume kisha akasema: “Samahani utamaduni wa Marekani ukaribisho kama huu kama kuna wanawake lazima nitaanza kuwahudumia, kisha wanaume. Ndio maana maji nimetangulia kuwapa hawa kinadada. Karibuni sana nimefurahi kuwaona.”

Baada ya stori za utambulisho za hapa na pale mahojiano yalianza ambapo alizungumza mambo mbalimbali ikiwemo namna anavyoshangaa kuona mgao wa umeme na maji nchini wakati ni mahitaji muhimu ya binadamu.

“Kitu kinachonishangaza ni maji na mvua zinanyesha. Ndio maana najiuliza kwa nini hayavunwi maji ya mvua? Umeme nao ni shida. Nimezoea baridi najikuta napata shida ndio maana hapa nyumbani pana jenereta angalau linapunguza makali.”

MAISHA TANZANIA Mchezaji huyo anasema joto ndilo linalomsumbua hapa nchini, lakini vitu vingine anavifurahia kama chakula, na anapenda kula chapati kwa maharage, wali maharage, pilau, biriani ila katika hivyo vyote anajua kupika mayai pekee.

“Kila kitu najifunza kidogokidogo. Baba yangu ndiye anayenisaidia kunifundisha kwa sababu ya mazoezi nakula chapati mbili hadi tatu asubuhi,” anasema. Nje na hilo, anasema maisha ya Tanzania kwa mara ya kwanza yalikuwa magumu hasa baada ya kutambulishwa kwenye timu na kitu kilichokuwa kinampa tabu ni lugha.

“Kabla sijaanza kuelewana nao (wenzake). Neno la kwanza kulishika lilikuwa tumechoka. Nilikuwa sijui wanamanisha nini, ila kwa sasa najua wanamanisha kuchoka mazoezi. Ukweli ni kwamba mazoezi ya Tanzania ni tafu kuliko Marekani.

Akiwazungumzia mastaa wa soka la nchini, Kaenda anasema: “Napenda wanavyocheza Saiki Atinuke, Precious Christopher kwa upande wa wanaume ni Aziz Ki. Anajua kupiga sana mashuti.”

STAILI YA KUSHANGILIA Kila akifunga bao mwanasoka huyo anapenda kushangilia kwa staili ya kufanya mazoezi na anaeleza kwamba staili hiyo hajaianzia Tanzania kwani katoka nayo Marekani kwenye kituo cha soka cha 7 Elite.

“Nilianza kufanya hivyo kwenye mazoezi ya kituo nilichokuwa najifunza kucheza,” anasema. Mchezaji huyo ni binti msomi anayesomea sayansi na michezo, lakini kwa mfumo huu.

“Nipo kidato cha sita. Marekani wanaangalia kama una akili unaruhusiwa kuomba chuo. Sasa nilishapata hiyo nafasi ya chuo, nikimaliza kidato cha sita namaliza na chuo kwa wakati mmoja.

“Nasomea mambo ya michezo. Nataka nije kuwa profeshono kocha. Niwe zaidi ya mama yangu maana ni kocha na kocha ninayempenda duniani ni Jurgen Klopp wa Liverpool. Huwa nafuatilia sana anachokifanya.”

Jambo linalomchekesha ni kitendo cha mashabiki kumuita Mzungu. “Nachukulia kama fani tu. Mimi ni Mtanzania kwa sababu baba yangu ni Mtanzania, ila mama ndiye Mzungu halisi,” anasema.

Wakati mashabiki wengi wa soka hapa nchini wanamuona kwa mara ya kwanza walikuwa wanamfananisha na straika wa Manchester City, Erling Haaland kumbe alikuwa anayasikia yote, lakini alijisikia furaha kuona anahusishwa na mtu mwenye mafanikio makubwa katika soka.

MSIKIE BABA YAKE Baba wa Kaeda, Reggie Wilson anasema lengo la kuja Tanzania na familia yake ni kujifunza maisha ili ajue yana tofauti gani na Marekani akiitaja hiyo kuwa ndiyo sababu ya kwanza ya binti yake kutokaa kambini.

“Mimi ni Mtanzania mama yake Mzungu, ila binti yangu anajivunia zaidi Utanzania. Nataka tupate uzoefu wa kimaisha kwa pamoja sasa akikaa kambini lengo langu halitatimia,” anasema.

“Sababu ya pili Marekani ni baridi sana tofauti na Tanzania. Ni joto kali hawezi kulala bila kiyoyozi, kwani feni hazimsaidii. Ishu nyingine ni chakula ambacho asilimia kubwa ni kigeni kwake, ingawa ameanza kukizoea.

“Jambo jingine ana umri mdogo. Ana miaka 18 ingawa ndani ya kikosi cha Yanga wapo wadogo kama yeye, ila kwa kuwa ni mtoto wangu wa kwanza. Lazima nimsimamie hadi nitakapoona akili yake imekomaa hizo ndizo sababu za kutokaa kambini.”

Anasema kama kunakuwa na programu ya mazoezi asubuhi anaondoka na bajaji kwenda kambini, kisha wanaelekea uwanjani.

“Akitoka uwanjani anarudi kambini anachukua usafiri wa bajaj kurudi nyumbani. Kwanza hatupo mbali na kambi ya Yanga Princess.”

Anasema binti yake ameanza kujifunza utamaduni wa Kitanzania na anaweza kufua na kufanya usafi kwa mikono tofauti na maisha ya Marekani ambayo wanatumia mashine. Mama yake mzazi, Shaylee Wilson anasema anafurahishwa kuona kipaji cha mtoto wake kinakua siku hadi siku na anaamini atafika mbali.

“Nguvu ya mimi na binti yangu kutimiza ndoto zetu za soka inatokana na sapoti kubwa ya mume wangu ambaye anatufuatilia kila tunachofanya na kutushauri,” anasema mzazi huyo ambaye binti yake alizaliwa mwaka 2006 U.H.A.T nchini Marekani na kabla hajajiunga na Yanga Princess alipita kwenye akademi ya 7 Elite iliyopo nchini humo.

Chanzo: Mwanaspoti