Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kadi ya bluu yazua gumzo

Blue Card Mean In Soccer Kadi ya bluu yazua gumzo

Sat, 10 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mapendekezo ya Bodi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (IFAB) ya kutambulisha kadi ya bluu katika soka la kulipwa kama sehemu ya majaribio ya kupunguza utovu wa nidhamu, yamezua mijadala mizito duniani kote ikiwamo Tanzania.

Mchezaji akionyeshwa kadi hiyo atatoka nje ya uwanja kwa dakika 10 na kisha kurejea mchezoni. Kadi hiyo itatolewa kwa makosa mawili tu, kufanya faulo (ambayo haikidhi vigezo vya kuonyeshwa kadi nyekundu) katika kuzuia mipango ya kuanzishwa kwa shambulizi na kupinga uamuzi wa waamuzi.

Atakayeonyeshwa kadi hii mara mbili katika mechi itakuwa ni nyekundu, sawa pia na ukionyeshwa njano na bluu katika mechi moja pia zinazaa kadi nyekundu.

Hii itakuwa rangi mpya ya kwanza ya kadi kutumika katika miaka 50. Matumizi ya kadi nyekundu na njano kwenye soka ndiyo yaliyozoeleka na yalianza kutumika mwaka 1970. Inasemekana matumizi hayo yalianzishwa na mwamuzi wa Uingereza, Ken Aston wakati wa Kombe la Dunia la FIFA huko Mexico.

Tangu wakati huo, kadi nyekundu na njano zimechukuliwa kama hatua sahihi zaidi kwenye soka za kumchukulia mchezaji na baadaye makocha duniani kote kwa wafanyao makosa ya kinidhamu uwanjani.

MTAZAMO TOFAUTI Mwamuzi wa zamani, Samwel Mpenzu alisema mapendekezo hayo kama yatapitishwa yanaweza kuziumiza timu nyingi za Ligi Kuu Bara na za madaraja ya chini lakini ni vyema kwanza kusubiri na kuona matokeo ya majaribio hayo kwenye ligi za wenzetu kama yatakuwa na matokeo mengi chanya au hasi.

"Jambo muhimu ni kujifunza kwanza kwa wenzetu kwenye majaribio ambayo wanaenda kuyafanya, kiukweli kabisa ni ngumu hilo kufanikiwa kwa mazingira ya mpira wetu wa Tanzania, labda itolewe elimu ya kutosha kwa wachezaji wetu, vinginevyo inaweza kuleta changamoto," alisema.

Pamoja na hilo wapo wadau wenye hofu ya mazingira ya upangwaji wa matokeo kuwa yanaweza kuwa rahisi kwani mwamuzi anaweza kuwachukulia hatua wachezaji fulani jambo ambalo linaweza kuiweka timu A katika mazingira magumu kwa muda ambao mchezaji huyo atakosekana.

Mahmoud Masoud ni miongoni mwao na hapa anaeleza, "Nimeifuatilia hiyo stori nadhani kwa wenzetu inaweza isiwe na shida sana lakini kwa mazingira ya mpira wa Tanzania ni wazi kuwa timu ndogo ndizo ambazo zinaweza kuumia, tunaujua mpira wetu huwa na mambo mengi nje ya uwanja."

Kwa upande wake, Israel Nkongo ambaye ni miongoni mwa waamuzi wabobezi ambao wamewahi kuchezesha mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga, anajua ilivyo presha ya mchezo huo ndani na nje ya uwanja. Alisema: "Hilo ni wazo tu, tusubiri kuona namna ambavyo watalifanyia kazi kabla ya kuanza kutumika, ikiwa rasmi na majaribio yake yakifanyika tunaweza kuongelea vizuri."

Kulingana na ripoti mbalimbali, Bodi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa imeeleza kwamba kadi hiyo itamfanya mchezaji kuondolewa kwenye mchezo kwa dakika 10 ikiwa atafanya makosa ya kuzuia shambulizi (ambayo hayakidhi kuonyeshwa kadi nyekundu) au kuonyesha kutokukubaliana na uamuzi wa mwamuzi wa mchezo husika.

Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema haoni kama mapendekezo hayo yanaweza kuwa na tija maana kama hatua za kinidhamu wachezaji wamekuwa wakichukuliwa kwa msaada wa hata VAR ikiwa mwamuzi atashindwa kuliona tukio hilo vizuri.

"Pengine inaweza kuwa utashi wa ligi kwenda na hilo kama ilivyo kwa VAR japo kwa kiasi fulani ni msaada kwa matukio tata, natamani kutafuta taarifa zaidi nisome ili nielewe nijue kusudi lao ni nini pengine naweza kuwa na mawazo tofauti ila sidhani kama ni sawa," alisema.

Majaribio ya hilo kwa mujibu wa taarifa mbalimbali yataanza msimu ujao ingawa hayatahusisha michuano mikubwa ya soka, ikiwemo zile ligi tano kubwa barani Ulaya, EPL, Serie A, Bundesliga, Ligue 1 na La Liga.

Majaribio hayo yanaweza kuchukua nafasi kwenye mechi za Kombe la FA kwa Wanaume na Wanawake huko England huku FA ikiripotiwa kukubali hilo.

Katika utaratibu huo mpya, ni nahodha tu ataruhusiwa kuzungumza na mwamuzi.

Kumekuwapo na wasiwasi kuhusu timu kupunguzwa nguvu na kubaki na wachezaji wachache uwanjani wakati wengine wakitumikia adhabu ya kuwa nje ya uwanja kwa dakika 10.

Staa wa zamani wa Arsenal na Real Madrid, Mesut Ozil, alitania kupitia ukurasa wake wa X, akiandika: "Kwa hiyo Atletico Madrid watacheza na wachezaji 6 sivyo?"

Maswali yanajitokeza itakuwaje katika mechi ya Simba na Yanga pale mwamuzi atakapowatoa nje wachezaji wanne wa timu moja katika dakika ya 80 kwa kosa la kumzonga?

Magwiji wa soka Ulaya, wamesema jambo hilo litaufanya mchezo wa soka uwe 'unaboa' zaidi kwani kila wachezaji watakapotolewa, wenzao watapaki basi ili kusubiri waliotolewa wamalize dakika 10 za adhabu na pia makipa watadanganya kuumia muda mwingi kuvuta dakika ili wenzao warudi uwanjani. Ukichanganya na dakika ambazo mchezo husimamishwa kuangalia VAR, soka linatarajiwa kuwa na vipindi vingi sana vya kusimama na timu kucheza kwa kupaki basi.

Kocha wa Tottenham, Ange Postecoglou, kocha wa Everton, Sean Dyche, na kocha wa Crystal Palace, Roy Hodgson ni miongoni mwa walioipinga kadi ya bluu huku gwiji wa Arsenal, Paul Merson akisema jambo hilo "litaua mchezo wa soka na kuufanya kuwa mchezo unaoboa zaidi."

Chanzo: Mwanaspoti