Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kadi nyekundu zaibua mjadala Ligi Kuu Bara

Kadi Pic Mwamuzi akimuonesha mchezaji kadi nyekundu

Fri, 5 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kwa wiki mbili kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) lakini kubwa la kushangaza kwenye ligi hiyo ni jinsi wachezaji wengi wanavyoendelea kupata kadi nyekundu.

Hadi sasa wachezaji nane wameonyeshwa kadi nyekundu wakati ligi ikiwa katika raundi ya tano, jambo ambalo linaonyesha kuwa msimu huu unaweza kuweka rekodi ya wachezaji kupata kadi nyingi.

Msimu uliopita hadi Ligi Kuu Bara inamalizika ni kadi nyekundu 21 tu zilitolewa, lakini msimu huu dalili mbaya zimeanza kuonekana mapema zaidi.

Wengi wanahoji je ni ukali wa waamuzi kushindwa kuwa wavumilivu au wachezaji wenyewe kustahili kutokana na makosa ya kizembe wanayofanya uwabjani?

Hadi sasa, Simba imekuwa timu ya kuogopwa zaidi na wapinzani kwani imesababisha kadi nyekundu nne kwa wachezaji wa timu pinzani, huku yenyewe ikiambulia moja.

Anwary Jabir wa Dodoma Jiji ndiye aliyeanza kuonja machungu ya Simba baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo baina ya timu hizo uliofanyika Oktoba 17 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Jabir alimpiga kiwiko beki wa Simba, Kennedy Juma wakati wakiwani mpira na kusababisha beki huyo kutoendelea na mchezo. Katika mchezo huo Simba ilishinda kwa bao 1-0.

Muhanga mwingine wa kadi nyekundu katika mechi dhidi ya Simba ni beki wa Poisi Tanzania, Juma Ramadhan, ambaye alipata kadi hiyo baada ya kumfanyia madhambi Benard Morrison eneo la hatari katika mchezo uliofanyika Oktoba 27, Uwanja wa Mkapa.

Kadi hiyo iliyotolewa dakika ya 90, pia ilizaa penalti kwa Simba, mkwaju ambao uliwekwa kimiani na Rally Bwalya na kuipa pointi tatu muhimu timu yake.

Mchezaji mwingine aliyepata kadi nyekundu katika mechi dhidi ya Simba ni Benedictor Mwamlangala wa Coastal Union, ambaye alipata kadi hiyo ya kujitakia dakika ya 74.

Benedictor akifahamu kuwa ana kadi ya njano, alichelewesha muda kwa kupiga mpira nje wakati tayari Henock Inonga akiwa ameshautenga kwa ajili ya kuuanzisha.

Lakini katika mchezo huo huo, Simba haikupona kwani dakika ya 90, Inonga alimpiga kichwa Issah Abushehe wa Coastal Union, tukio ambalo lilisababisha aonyeshwe kadi nyekundu ya moja kwa moja.

Novemba 3, Abdulaziz Makame wa Namungo naye akajikuta akiingia katika mkosi wa kadi nyekundu kwa timu zinazocheza dhidi ya Simba.

Kiungo huyo wa zamani wa Yanga alijikuta akiwagharimu wenzake baada ya dakika ya 51 kumchezea madhambi, Shomari Kapombe na kusababisha kupata kadi nyekundu.

Namungo ambayo ilicheza pungufu muda mwingi wa mchezo ilijikuta ikizidishiwa machungu baada ya kuruhusu bao dakika ya 94 liilofungwa kwa kichwa na Meddie Kagere.

Wachezaji wengine walioonyesha kadi nyekundu kwenye Ligi Kuu hadi sasa ni Joseph Majagi wa Mbeya Kwanza aliyeonyeshwa kadi katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji uliofanyika Oktoba 17 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, baada ya kumuangusha Agustino Nsata eneo la hatari wakati wakiwania mpira.

Beki Ismail Gambo wa KMC naye ameingia katika kitabu cha waliopata kadi nyekundu za mapema msimu huu baada ya kuo yesha kadi katika mchezo dhidi ya Coastal Union uliofanyika Oktoba 4, huku beki wa Ruvu Shooting, Santos Mazengo naye alipata kadi nyekundu Novemba 2 baada ya kumsukuma mshambululiaji wa Yanga, Fiston Mayele wakati akielekea kufunga.

Mwamuzi wa zamani, Othman Kazi alisema msimu huu kadi zinzweza kwa nyingi kutokana na ushindani mkubwa kwa timu shiriki kwani wachezaji wameonekana wamepania.

“Kwanza hela zilizowekwa na Azam zimesababisha timu nyingi kupambana sana uwanjani na ndiyo maana unaona hata mabao yamepungua. Hivi vitendo vya rafu za mara kwa mara zinazosababisha kadi zinakupa picha jinsi wachezaji walivyopania kutokana na fedha nyingi iliyowekwa kwenye ligi msimu huu.

“Lakini kubwa ni kutozijua sheria kwa wachezaji, kwani wengi sheria zinawatatiza. Unaweza kufanya kosa na wasijue madhara yake, hivyo lazima wachezaji wazijue sheria za soka ili wajue madhara ya makosa wanayofanya uwanjani,” amesema Kazi.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz