Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kabwili aongeza petroli moto wa rushwa Simba

93718 Kabwili+pic Kabwili aongeza petroli moto wa rushwa Simba

Thu, 30 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika moto ulioonekana kuanza kufifia, Ramadhani Kabwili wa Yanga ameongeza petroli baada ya kuibua tuhuma za jaribio la kiongozi mmoja wa klabu pinzani ya Simba kumhonga ili akose mechi ya watani hao wa jadi.

Kabwili ameongeza idadi ya tuhuma za rushwa dhidi ya viongozi wa Simba katika kipindi kisichozidi miaka kumi.

Kwa kipindi hicho cha kuanzia mwaka 2010, Simba ilitwaa ubingwa kwa mara ya mwisho msimu wa 2011/12 na haikutwaa tena ubingwa hadi msimu uliopita.

Matukio mengine ya tuhuma za rushwa yalimuhusisha Ulimboka Mwakingwe, aliyekamatwa na polisi mjini Morogoro kwa tuhuma za kutumwa fedha za kumpelekea kipa Shabani Kado wa Mtibwa. Nyingine zilihusu wachezaji watatu wa Azam-- Deogratius Mushi ‘Dida’, Said Morad na Aggrey Morris waliosimamishwa kwa tuhuma za kula njama na kiongozi wa Simba ili kuihujumu timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara.

Jingine lilimuhusu kiungo wa zamani, Pius Kisambale ambaye pia alidai alipigiwa simu na kiongozi mmoja wa Simba aliyemtaka acheze chini ya kiwango kama angepangwa na kumuahidi kumpa pesa na kama angeweza aongee na wachezaji wengine wa Yanga kuhusu mpango huo, sawa na Nsa Job ambaye alidai aliahidiwa fedha ili asiwafunge mabingwa hao watetezi wa Bara.

Tuhuma tatu kati ya hizo zinahusu makipa Kabwili, Kado na Dida wakati mengine mawili yanamuhusu mshambuliaji Nsa na kiungo Kisambale.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Suala la Nsa lilifikia TFF na kwa mujibu wa taarifa za wakati huo lilikuwa likisubiri kufikishwa mbele ya Kamati ya Maadili lakini haikufanyika, wakati suala la wachezaji wa Azam lilifika ofisi za Takukuru wilayani Temeke huku suala la Ulimboka likiishia kituo cha polisi Morogoro na la Kisambale likiishia makao makuu ya Takukuru.

Wakati tuhuma hizo tatu zikionekana kuanza kufifia, Kabwili ameuweka upya uongozi wa Simba katika wakati mgumu baada ya kueleza katika mahojiano jaribio la kutaka kurubuniwa na kiongozi mmoja wa klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.

Alisema msimu uliopita wakati Yanga ikijiandaa kucheza na Simba, kiongozi mmoja wa klabu hiyo kongwe alimshawishi afanye vitendo vitakavyosababisha aonyeshwe kadi ya njano na hivyo kufikisha tatu mfululizo, ambazo kikanuni zingemlazimisha akose mechi iliyofuata dhidi ya Simba.

Mbali na fedha, Kabwili amedai aliahidiwa kupewa gari aina ya Toyota IST.

Kabwili amedai kuwa wakati huo kipa namba moja, Beno Kakolanya, ambaye kwa sasa anaichezea Simba, alikuwa na matatizo, hivyo waliamini kipa wa pili, Klaus Kindoki ni rahisi kumfunga na ndio maana wakamtaka kipa huyo chipukizi asiwepo.

Tayari Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka (TFF) imemuita kipa huyo chipukizi kwa ajili ya mahojiano, jambo ambalo kwa sasa linamzuia kuzungumzia zaidi tuhuma alizozitoa redioni.

“Kauli hizi zina madhara makubwa katika uadilifu wa viongozi na klabu,” alisema Senzo Masingiza, ofisa mtendaji mkuu wa Simba.

Mbali na Senzo, hakuna kiongozi mwingine wa Simba aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo, huku Ismael Rage, ambaye alikuwa kiongozi wakati wa tuhuma dhidi ya Dida na wenzake, akisema hataki kuzungumza lolote.

Ulimboka, ambaye kabla ya tuhuma hizo alikuwa mchezaji wa Simba, hakutaka kuzungumzia tukio hilo.

Naye Crescentius Magori, ambaye alikuwa mtendaji mkuu wa muda wa Simba alijikita katika kuhoji ukweli wa tuhuma hizo.

“Amemtaja mtu aliyetaka kumhonga? kipindi hicho alichotaka kuhongwa mimi ndiye nilikuwa CEO Simba, mbona hilo jambo sikulisikia,” alisema Magori.

Wadau

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Idd Kipingu alisema matukio kama hayo yanafanywa na watu wenye nia ya kuharibu soka.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau alipoulizwa alisema suala la Simba na Kabwili liko kwenye kamati linashughulikiwa. Kabwili alipoulizwa alisema hawezi kulizungumzia sababu ameitwa kamati ya maadili kutoa maelezo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo alisema tuhuma hizo wanazifanyia kazi na watawaita wahusika wote kuwahoji.

Chanzo: mwananchi.co.tz