Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaburu arejesha fomu Simba

Kaburu Pic Data Aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti wa klabu ya Simba, Geodfrey Nyange 'Kaburu'

Mon, 19 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kama ulikuwa unadhani Makamu wa Rais wa zamani wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ anabipu kwenye mbio za kutaka kurejea madarakani, basi pole yako, kwani kigogo huyo hatanii baada ya Ijumaa iliyopita kuwa mgombea wa kwanza kurejesha fomu za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.

Kaburu, amejitosa kuwania nafasi ya uenyekiti na ndiye pekee kati ya watatu waliochukua fomu za uchaguzi huo kurejesha fomu.

Kaburu alirudisha fomu hiyo, huku wagombea wengine wawili wa nafasi hiyo, Yusuf Majid Nassor na Yusuf Omary Yenga aliyechukua pia fomu ya kugombea ujumbe walikuwa hawajarudisha.

Kaburu aliwahi kuwa makamu mwenyekiti wa Simba wakati Rais akiwa Evance Aveva.

Mgombea mwingine aliyerudisha fomu hizo ni, Injinia Rashid Khamis aliyekuwa amechukua fomu mbili za uenyekiti na ujumbe, lakini alirudisha ile ya ujumbe tu na kuachana na nafasi ya mwenyekiti.

Uchukuaji na urudishaji wa fomu hizo utafungwa kesho Jumatatu saa 10.30 jioni kwenye ofisi za klabu hiyo zilizopo Oysterbay, jijini Dar es Salaam.

Hadi jana Jumamosi waliochukua fomu za kuwania ujumbe ni; Abubakari Zebo, Abdallah Rashid Mgomba, Hawa Mwaifunga, Iddy Kajuna, Laurian Mganga, Elisony Edward Mweladzi, Lameck Lawrence, Nadir Atul, Omary Juma Mazora, Andala David Sizya, Christopher Kabalika Mwansasu, Hassan Bakar Kakayo, Isihak Ashraf Mukadamu, Seleman Haroub Said, Sharing Jumbe, Aziz Mohamed, Amina Ngaluma, Issa Masoud Idd, Hudhaifa R Kassim na Penda A Mapugilo.

Hata hivyo, Mwanaspoti linakupa dondoo kwa mujibu wa Katiba ya klabu hiyo inayozungumzia mambo ya uchaguzi.

Ibara ya 27: Sifa za

Wagombea

1. Kutakuwa na wajumbe wanane (8) watakaoiwakilisha Simba Sports Club katika Bodi ya Wakurugenzi; sita (6) wa kuchaguliwa na wawili (2) wa kuteuliwa ambao kati yao: -

(a) Mjumbe mmoja atachaguliwa kama mwenyekiti na ni lazima awe na taaluma kiwango cha chini cha elimu ya angalau shahada ya kwanza au sifa inayolingana na hapo kutoka Chuo Kikuu kinachotambulika na Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

(b) Mjumbe mmoja (1) lazima awe na taaluma kiwango cha chini cha elimu ya angalau shahada ya kwanza au sifa inayolingana na hapo kutoka Chuo Kikuu kinachotambulika na Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

(c) Wajumbe wengine wanne (4) wa kuchaguliwa waliobaki wanatakiwa kuwa na elimu isiyopungua kidato cha nne na angalau mjumbe mmoja wapo kati yao awe mwanamke.

(d) Wajumbe wawili (2) watateuliwa na mwenyekiti kutoka miongoni mwa wanachama ambao ni lazima wawe na taaluma ya angalau kidato cha nne.

2. Mtu yeyote anayegombea nafasi yeyote ya Simba Sports Club, hana budi kutimiza masharti yafuatayo:

i. Awe na sifa zinazotakiwa kwa nafasi husika na amelipa ada ya uanachama kikamilifu tangu alipoanza uanachama.

ii. Awe na kiwango cha chini cha elimu kama ilivyoainishwa katika ibara ya 27 (1) (a)(b) na (c). iii. Kiongozi wa kuchaguliwa atakaa madarakani kwa vipindi viwili tu vya kupiga kura kwa nafasi ya uongozi. Endapo atataka kurejea madarakani baada ya kutumikia vipindi viwili mfululizo, itabidi asubiri kwanza kupita kwa walau uchaguzi mkuu mmoja wa kikatiba.

iv. Asiwe aliyewahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai kwa kuhukumiwa kifungo.

v. Awe na umri angalau miaka 25.

vi. Awe ametimiza angalau miaka mitatu ya uanachama.

vii. Asiwe mwamuzi wa mchezo wa Mpira wa miguu anayefanya shughuli za uamuzi kwa kipindi hicho.

viii. Mwanachama mwenye umri wa Miaka 65 na kuendelea hataruhusiwa kugombea.

Chanzo: Mwanaspoti