Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaburu: Mafisango alikuwa mtu sana

Kaburu Pic Data Godfrey Nyange "Kaburu"

Wed, 17 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Leo ni miaka 11 tangu kiraka wa Simba, Patrick Mutesa Mafisango afariki dunia kwaajali ya gari eneo la Keko, Jijini Dar es Salaam na kuzikwa kwao Gombe, Kinshasa. Ni msiba ambao uliacha pengo kwa Simba lakini kwa timu yake ya Taifa ya Rwanda Amavubi. Mpaka leo akiwa amepumzika kaburi, hakuna anayeamini kilichotokea zaidi ya kumuombea kwa Mungu aendelee kupumzika kwa amani.

Simba ilikuwa moto chini ya kiungo chake ikiwa kwenye utawala wa Mwenyekiti wa wakati huo, Ismail Aden Rage huku makamu wake akiwa Geofrey Nyange Kaburu.

Ukiwauliza viongozi wa zamani wa Simba kiongozi gani alikuwa karibu sana na Mafisango watakutajia Kaburu ambaye alikuwa mmoja wa watu walioshiriki kwa karibu wakati huo kusimamia usajili wa kiungo huyo mwenye asili ya DR Congo kuja Simba akitokea Azam FC na hapa anaelezea maisha yalivyokuwa wakati huo.

ALIVYOTUA NA ALIVYOIJULIA

"Unajua Mafisango alikuja Simba akiwa na mkataba, hakufurahishwa na maisha ya Azam FC tangu alipofika akaomba kuondoka na sisi tuliona kipaji chake tukakaa mezani na Azam wakatupa masharti tuwape Abdulhalim Humoud ili wao watupe Mafisango, tukaona ni sawa, kwa hiyo alikuja kwetu akiwa na mkataba nusu wa Azam.

"Alipokuja Simba akawa amekuja na bahati akaonyesha kiwango bora sana na mashabiki wakamkubali sana ndio tukaanza kuongea naye ili aongeze mkataba zaidi wa kubaki kwetu,"anasema.

Licha ya kuonekana kama hana nidhamu, Kaburu anafichua Mafisango alikuwa na msaada mkubwa kwa wachezaji wenzake ambao nao walikuwa wanaonekana wasumbufu wakati huo.

"Kulikuwa na kundi maalum la kina Mafisango katika timu yetu nakumbuka alikuwa yeye (Mafisango), Redondo, Kazimoto (Mwinyi), Boban (Haruna Moshi), Maftah (Amir), Nyosso (Juma), Sunzu (Felix) hao watu nadhani unawaona hapo utamuongeza na Kaseja (Juma) na Okwi (Emmanuel) ambaye yeye alikuwa mwenzao lakini sio kama hao wengine.

"Hili lilikuwa kundi gumu sana wakati huo, tulikuwa tunawachukulia kama watovu wa nidhamu ingawa walikuwa wakiingia uwanjani lazima utaumia wanafanya kazi kubwa.

"Kitu ambacho kilikuwa tofauti, Mafisango ndio alikuwa anasikilizwa zaidi na wenzake na alikuwa na kauli ya kujua jinsi ya kututuliza viongozi, kama anaona mwenzake amekosea atakuja kwetu na kumwombea msamaha huku akiahidi kumbadilisha, tukawa tunaona juhudi zake,"anasema.

MAISHA YAKE YA MWISHO

"Unajua wakati msimu wa 2011/12 ulikuwa umemalizika tukiwa tunatoka kucheza na Al Hilal Shandy ya Sudan, mimi niliwahi kurudi na timu ikarejea siku mbili baadaye, sasa Mafisango wakati timu inarejea akapigiwa simu amechaguliwa kujiunga na timu ya taifa ya Rwanda, yule alikuwa amechukua uraia wa Rwanda ingawa ana asili ya Kongo."

"Wakati huo tulishakubaliana anatakiwa kuongezewa mkataba baada ya kuridhika na kiwango chake, alinipigia simu na kunieleza juu ya huo wito nikamwambia awali ya yote nataka kuonana naye, tukakubaliana nimfuate kwake Chang'ombe ambako tulikuwa tumewapangia wachezaji wetu wote.

"Kesho yake kweli nilifika kule nikamkuta amekaa nyumbani akiwa na wachezaji wenzake akiwemo rafiki yake sana wakati huo Redondo (Ramadhan Chombo), nikamuita tukaongea akaniunganisha na watu wa Rwanda nao wakanithibitishia juu ya huo wito nikawapa barua pepe wakatuma huo mualiko kwa hiyo tukafanya maamuzi ya kumruhusu."

KUMBE YANGA WALIMTAKA

"Tulipomaliza hilo tukaanza kuongelea suala la kumwongeza mkataba, hapo akanieleza wazi anapata usumbufu mkubwa na watu wa Yanga ambao kumbe walikuwa wanamtaka, akanionyesha hadi mawasiliano yake na wao lakini nikamwambia Simba inataka kumbakisha na akakubali, akataka kujua ofa yetu, nikampa tukakubaliana tumuache aende kwanza kwao Congo anataka kwenda kusalimia familia yake kisha akitoka huko atarudi Rwanda kujiunga na timu ya taifa na akimaliza majukumu ya timu ya taifa atakuja Tanzania ili asaini mkataba mpya.

"Unajua kitu kilichokuwa kinamsukuma Mafisango ni marafiki zake wengi walikuwa hapa Simba, alikuwa anafikiria akienda Yanga ataanza maisha mapya na hata wakati natoka pale kwake tunaachana Redondo alinisisitiza ni muhimu Mafisango tumbakishe nikawaachia fedha za kuburudika nikawaacha manaa aliniambia wanataka kufurahi hizo siku mbili kabla ya kuondoka."

SIMU YA ALFAJIRI

"Nilipoondoka kesho yake saa kumi na moja alfajiri nikapigiwa simu, nilishtuka maana sikuwahi kupata simu za Simba nyakati kama hizo, nilipopokea nikajulishwa Mafisango amepata ajali mbaya na amefariki.

"Niliona kama niko kwenye ndoto, nilikataa lakini sikupuuza nikatoka maana niliambiwa mwili wake unapelekwa Muhimbili, nilitoka haraka na kuwahi Muhimbili, nilipofika nikakuta ndio ameingizwa chumba cha kuhifadhia maiti.

"Nilitaka nijiridhishe na wakaniruhusu, niliumia sana nilipothibitisha kweli Mafisango ametangulia, niliishiwa nguvu kwa kweli na alikuwa ameumia zaidi kichwani, baada ya hapo nikaanza kuwajulisha wenzangu na kuwathibitishia na taratibu zingine kufuata." Mafisango alifariki Mei 17, 2012. Tarehe kama ya leo.

AZAM ILIWAZIDI

Kaburu anaeleza kumbe Mafisango angetua Simba kabla ya kwenda Azam, lakini alipigwa bao na rafiki yake ambaye alikuwa bosi wa Azam FC, Patrick Kahemele ambaye aliwahi kumalizana naye.

"Mafisango angetua Simba hata kabla ya kwenda Azam, labda niwafahamishe watu mara ya kwanza nilipata taarifa kuna mchezaji mzuri sana kiraka anayejua kucheza nafasi za beki wa kati, beki wa kushoto na kiungo wa kati boksi tu boksi.

"Yalikuja mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati yalifanyika Rwanda na Mafisango alikuwa anaichezea APR nikaenda kule kumfuatilia, nilipokuwa kule nilikutana na rafiki yangu Kahemele (Patrick) kwa hiyo tulikuwa pamoja, sasa wakati tunaangalia zile mechi na yeye akamuona Mafisango kila mmoja akawa anamuwinda kivyake, moyoni kwake sasa wakati tunajipanga wenzetu wakafanya maamuzi ya haraka wakatuwahi na kumsajili basi tukawa Simba tumepigwa bao kwa wakati huo."

KIKOSI CHA 5-0 DHIDI YA YANGA

Kaburu anaeleza kuwa Mafisango amewaachia ari ya kupambana kwa hamasa yake binafsi pamoja na uwezo wake wa kuhamasisha wenzake kushinda. Alichangia kiasi kikubwa ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Yanga.

"Ile mechi nakumbuka alikuwa ndiye mhamasishaji. Wakati wa mchezo wote tulikuwa juu tunamuona anavyowahamasisha wenzake kutamani ushindi mkubwa. Kila alipowaona wenzake wanaanza kupunguza kasi aliwasisitiza kupambana kwa nguvu.

"Kitu bora zaidi hata yeye mwenyewe alifanya kazi kubwa, alicheza sana siku hiyo, ndiyo maana ilipotokea penalti walimpa afunge lakini hatukujua kumbe ndio alikuwa anatuachia kumbukumbu ya maisha yake. Hakika alikuwa hazina kubwa kwa klabu yetu na Wanasimba walithamini kipaji chake na wakashiriki kwa wingi kumuaga kabla ya kusafirishwa." Apumzike kwa Amani.

Chanzo: Mwanaspoti