Kipa Andre Onana amesema yupo tayari kupokea lawama zote za Manchester United kufanya vibaya.
Onana, 28, ni mmoja wachezaji wenye majina makubwa kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.
Timu hiyo imemaliza msimu vibaya, ikishika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Lawama kubwa zimeelekezwa kwenye safu ovyo ya ulinzi ya timu hiyo na Man United iliruhusu kupigiwa mashuti 660 msimu huu, ikiwa timu ya pili ikizidiwa na Sheffield United pekee.
Onana alisema hilo limetokana na majeruhi wengi kuiandama safu yao ya ulinzi.
Wakati akitambua timu inapaswa kufanya vizuri, wasiwasi wake ni lawama hizo zitakwenda kwa wachezaji makinda kwenye timu, zitawaathiri kisaikolojia.
Onana, lawama zote zinapaswa kuelekezwa kwake na wachezaji wengine wakubwa kwenye kikosi hicho kama Bruno Fernandes, Casemiro na Harry Maguire.
Alisema: “Kwa upande wangu, wala sijali. Nimekuja kwenye hii timu kukubali kukosolewa kwa sababu bado ipo kwenye mapito ya kujijenga upya. Hatuko vizuri kwa sasa. Kuna timu nyingine zipo vizuri kutuzidi, hilo tunalitambua.
“Basi kama mambo hayakwenda hovyo, msiwashambulie wachezaji vijana, mimi nipo, Bruno (Fernandes), Casemiro na Harry (Maguire) tupo, tumeshazoea lawama. Mimi sijali, naona ni sehemu ya mchezo.”
Licha ya kupigiwa mashuti mengi hivyo, Onana ameruhusu mabao 58 huku akiwake wastani wa asilimia 74.9 ya kuokoa hatari, ikiwa ni bora zaidi Ligi Kuu England.
Man United haikuruhusu bao kwenye mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu England dhidi ya Brighton na Onana aliokoa hatari nyingi kwelikweli kufikisha mechi yake ya tisa bila ya wavu wake kuguswa.
Man United imebakiza mechi moja, fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester City itakayopigwa Mei 25.