Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Mastaa wa Afrika wa kuchungwa

Qatar Pic Data Nyota wa Senegal, Sadio Mane

Wed, 28 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, mataifa matano yatakayoshiriki yatakuwa na mastaa wakali kutoka maeneo tofauti duniani. Mastaa hawa wanatarajiwa kuzibeba timu zao kutokana uwezo na uzoefu ambao wamekuwa nao katika soka la ushindani.

Hapa, tunakuletea rekodi kamili na mafanikio ya wachezaji wote ambao wanaweza kuzibeba timu za Afrika katika fainali hizi.

SADIO MANE

Licha ya ugeni wake kwenye kikosi cha Bayern Munich ameendeleza moto uleule aliouonyesha akiwa na Liverpool.

Jamaa ni mmoja kati ya wachezaji wa kuchungwa sana kwenye kikosi cha Senegal kutokana na ubora aliouonyesha kwenye michezo ya kufuzu na Mashindano ya Afcon.

Hii itakuwa ni mara yake pili kushiriki fainali hizi za Kombe la Dunia, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 2018 kule Urusi. Mane ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Timu ya Taifa ya Senegal akiwa na mabao 34 aliyofunga kwenye mechi 92 ambazo pia zimemfanya kuwa mchezaji namba tatu kwa kucheza mechi nyingi za taifa hilo.

Ameshinda karibia mataji yote makubwa akiwa na Liverpool kwa ngazi ya klabu. Ndiye staa wa Senegal, ni mchezaji atakayesumbua sana.

EDUARDO MENDY

Hii inakuwa ni mara yake ya kwanza kucheza fainali hizi. Msimu huu haujawa mzuri sana kwake akiwa na Chelse ambapo amecheza mechi sita za Ligi Kuu England na kuruhusu mabao tisa.

Hata hivyo, hiyo haiondoi ukweli kwamba amekuwa mmoja kati ya makipa bora na hata kwenye AFCON alionyesha kiwango bora hadi akaisaidia Senegal kufika fainali. Uzoefu alioupata akiwa na Chelsea kwenye michuano ya kimataifa utakuwa silaha kubwa katika fainali hizi.

HAKIM ZIYECH

Staa wa kimataifa wa Morocco, amecheza jumla ya mechi 41 za michuano mbalimbali akiwa na timu hii ya taifa. Alilishiriki Kombe la Dunia kule Urusi. Msimu huu hajapata nafasi kubwa ya kucheza kwani hadi sasa ameonekana kwenye mechi nne tu akiwa na Chelsea mbili za ligi na mbili za Ligi ya Mabingwa.

Hata hivyo, bado anabakia kuwa mchezaji hatari kwenye kikosi hicho kutokana na historia yake na uwezo aliouonyesha kwenye misimu kadhaa katika soka la ushindani.

Katika mechi 41 alifunga mabao 17 ambayo mengi yalitokana na mechi za kirafiki ambako amefunga mabao manane.

Fainali za Kombe la Dunia amecheza mechi tatu pekee ambazo ni za hatua ya makundi.

ACHRAF HAKIMI

Staa mwingine wa Morocco. Ni miongoni mwa mabeki bora sana kwenye soka la Ufaransa, amekuwa mchezaji tegemeo wa PSG kwa muda mrefu na kujihakikishia namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.

Msimu huu pia umekuwa mzuri kwake kwani hadi sasa amecheza mechi 11 za michuao yote, akifunga mabao mawili na kutoa asisti mbili.

Jamaa amekuwa na uwezo mkubwa wa kufunga na kutoa asisti jambo ambalo huziweka timu nyingi kwenye hatari pale anapocheza eneo la beki wa kulia ambalo ndio alilolizoea. Kwa ujumla amecheza mechi 51 akiwa na taifa hili na akafanikiwa kufunga mabao manane na kutoa asisti saba.

Alikuwepo kwenye kikosi cha timu hii kilichocheza michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na akacheza mechi zote tatu za hatua ya makundi.

THOMAS PARTEY

Waingereza wanamuita ‘Octopas’ kwa maana ya Pweza, ni kutona na aina ya uchezaji wake, jinsi anavyogawa mipira pande zote pale anapokuwa eneo la katikati ya uwanja.

Kwenye mechi za kufuzu michuano hii jamaa alifunga mabao matatu katika michezo minne.

Bao lake dhidi ya Nigeria kwenye sare ya bao 1-1 ndio liliipa nafasi Ghana kushiriki fainali za mwaka huu.

Kwa sasa anasumbuliwa na mejaraha lakini ikipona atakuwa msaada mkubwa kwa Ghana kutokana na uwezo wake.

Ameshacheza mechi 38 za timu hii ya taifa na kufunga mabao 12 na asisti sita.

Kwa sasa ni mmoja kati ya viungo bora na tegemeo kwenye kikosi cha Arsenal.

Hii itakuwa ndio mara yake ya kwanza kushiriki fainali hizi za Kombe la Dunia. Lakini hiyo haiwezi kuwa tabu kwani ana uzoefu wa kucheza michuano mbalimbali mikubwa.

Msimu huu hakuanza vizuri akiwa anaitumikia Arsenal kutokana na majeraha yanayomuandama, lakini bado ni miongoni mwa wachezaji hatari zaidi kwani mbali ya jukumu lake la kuwa kiungo wa kati au mkabaji, bado amekuwa na uwezo mkubwa wa kufunga kwa kutumia njia mbalimbali, vilevile amekuwa akitoa asisti.

ANDREW AYEW

Staa mwingine wa kimataifa wa Ghana. Ni miongoni mwa wachezaji wachache kwenye kikosi hiki ambao walikuwepo kwenye fainali hizi, akicheza jumla ya mechi saba, kuanzia ile ya mwaka 2010 hadi 2014.

Ayew ndio kapteni wa Ghana kwa sasa na anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa pili kwa kucheza mechi nyingi zaidi akiwa amecheza mechi 107 nyuma Asamoah Gyan ambaye amecheza mechi 108.

Ayew amefunga mabao 23 katika mechi hizo, kwa sasa hayupo kwenye soka la ushindani sana kwania anacheza huko Saud Arabia.

Lakini uzoefu wake kwenye michezo ya kimataifa inaweza kuwa silaha kubwa kwa Ghana. Ni mshambuliaji mzuri asiyekata tamaa.

WAHBI KHAZRI

Huyu ni staa wa kimataifa wa Tunisia. Kwa sasa anaitumikia Montpellier ya Ufaransa, ndio mfungaji bora namba mbili wa timu hii akiwa na mabao 34, ndiye mhimili muhimu wa timu hii kwenye sekta ya ufungaji.

Alikuwepo kwenye kikosi cha Tunisia kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia kule nchini Urusi ambapo alifunga mabao mawili na kutoa asisti mbili kwenye mechi tatu.

Kwenye mechi sita za kufuzu fainali hizi ambazo staa huyu amecheza, alifunga jumla ya mabao matatu na baadhi ya mechi alizikosa kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

Uzoefu wake na ubora wake unatarajiwa kuwasaidia sana Tunisia kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, pia ndiye anayetarajiwa kuwa mchezaji hatari zaidi.

VINCENT ABOUBAKAR

Miongoni mwa wachezaji waliofanya kazi kubwa sana kuisaidia Cameroon kutwaa taji la AFCON mwaka 2017. Ndiye kapteni wa sasa wa timu hii akiwa amecheza jumla ya mechi 88 na kufunga mabao 33.

Yupo kwenye 10 bora ya wafungaji wa muda wote wa timu hii, kwenye fainali za AFCON mwaka huu, alimaliza akiwa mfungaji bora kwa mabao yake 10.

Ana uzoefu mkubwa na fainali hizi kwani ameshiriki kwa njia moja ama nyingine. Mwaka 2010 kule Afrika Kusini hakupata nafasi kubwa ya kucheza kutokana na wingi wa mastaa waliokuwepo kwenye kikosi kwa wakati huo na yeye hakuwa na uzoefu wa kutosha. Alianza kutumika kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014.

Ubora wake na uzoefu wake katika fainali hizi unaonyesha jamaa atakuwa msumbufu sana kwa safu za ulinzi za timu pinzani.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz