Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KMKM yaua, hat-trick ya pili yafungwa Zenji

KMKM Yaua KMKM yaua, hat-trick ya pili yafungwa Zenji

Thu, 2 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) imezidi kunoga baada ya watetezi wa ligi hiyo KMKM jana jioni kuifyatua New City kwa mabao 5-0, huku nyota wake, Ibrahim Isakah akifunga hat trick ikiwa ni ya pili kwa msimu huu na kumfanya aongoze orodha ya wafungaji wa ligi hiyo akifikisha mabao matano.

KMKM ilipata ushindi huo mnono kwenye Uwanja wa Mao Zedong A, mjini Ugunja, ukiwa ni wa pili kushuhudiwa kwenye ligi hiyo kwa msimu huu, baada ya ule wa Zimamoto iliyoicharaza Ngome FC pia kwa mabao 5-0, huku nyota wake Ibrahim Hamad 'Hilika' akipiga hat trick iliyojibiwa juzi na wajina wake, Ibrahim Isakah.

Ushindi huo umeifanya KMKM kuchupa kutoka nafasi ya saba hadi ya tatu kwa kufikisha pointi 13 baada ya kushuka uwanjani mara saba, huku KVZ na JKU zikiwa juu kwa kila mmoja kukusanya pointi 16, ila zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Katika mechi hiyo ya juzi, Ibrahim Isakah alianzisha balaa mapema kwa kufunga bao la kwanza dakika ya kwanza tu ya mchezo na wakati wageni wa ligi hiyo New City wakijiuliza jinsi ya kulirudisha, wakajikuta wakifungwa tena la pili na mfungaji huyo huyo katika dakika ya 22.

Salum Shukuru aliifungia KMKM bao la tatu dakika ya 30, likiwa ni la tatu katika ligi hiyo hadi sasa na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 3-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko, lakini ni KMKM iliyonufaika nayo baada ya Ibrahim kufunga tena bao dakika ya 57, likiwa ni la tatu kwake na kukamilisha hat trick, huku likiwa ni la nne kwa timu hiyo inayoshikilia taji la ZPL kwa msimu wa tatu mfululizo.

New City ilijitahidi kujitutumua kusaka angalau lao la kufutia machozi, lakini umakini mdogo wa washambuliaji wake, uliwaangusha na dakika saba kabla ya pambano hilo kumalizika Makame Kheri alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la timu hiyo kwa kufunga bao la tano la KMKM.

Ligi hiyo itaendelea tena jioni ya leo kwa mechi mbili za kukamilisha raundi ya saba, wakati vinara KVZ itakuwa wageni wa Ngome FC kwenye Uwanja wa Mao A, huku Uhamiaji itaikaribisha Malindi katika Uwanja wa Mao B.

Chanzo: Mwanaspoti