Baada ya kunusurika kushuka daraja, mabosi wa KMC jana Jumatano walikutana kujadili msimu mzima ulivyokuwa ikiwa ni pamoja na kupanga mipango ya msimu ujao ikiwemo usajili na kocha mkuu.
Mabosi hao ambao wanaunda Bodi ya Wakurugenzi walifanya tathmini ya kikosi chao ambacho hakikuwa na mwenendo mzuri msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara huku wakinusurika kushuka baada ya kuifunga Mbeya City kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye mchezo wa mtoano Play Off.
Katika mchezo wa kwanza wa play off ambao KMC walicheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, KMC ilifungwa mabao 2-0 wakati marudiano iliyochezwa Uwanja wa Uhuru, ilishinda mabao 2-0, hivyo KMC ilibaki kwa ujumla ya mabao 3-2.
Katika kikao hicho pia imeelezwa walijadili juu ya mkataba wa kocha wao Jamhuri Kihwelo 'Julio' ambaye alipewa mkataba wa miezi mitatu baada ya kuachana na Theirry Hitimana katikati ya msimu.
Mwanaspoti lilimtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa KMC, Daniel Mwakasungula ili kuelezea mipango yao baada ya kunusurika kushuka daraja alisema kila kitu kitatolewa ufafanuzi hapo baadaye.
"Msimu ulikuwa mgumu kwetu hadi tulifikia hatua ya kucheza play off, tunashukuru tumebaki sasa ni kujipanga lakini ikumbukwe kwamba hii ni timu ya Halmashauri ambapo kuna taratibu zake, hivyo kila kitu kitatolewa ufafanuzi kwa kufuata utaratibu wetu," alisema Mwakasungula.