Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KMC yaingia kambini kuzisaka alama tatu za Mtibwa

DCE376F6 306B 47B8 A0DF AA86984AA567.png Wachezaji wa KMC

Tue, 11 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha KMC FC jana Jumatatu (Oktoba 10) kimeanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Jumamosi (Oktoba 15) katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni inayonolewa na Kocha Mkuu Thierry Hitimana iliingia kambini juzi Jumapili (Oktoba 09) jioni, baada ya mapumziko ya siku mbili tangu ilipocheza mchezo wa mzunguko wa sita dhidi ya Ruvu Shooting na kuambulia sare ya kutokufungana.

KMC FC inajiandaa na mchezo huo ikihitaji ushindi baada ya kutoa sare katika michezo miwili dhidi ya Namungo FC iliyocheza katika Uwanja wa Majaliwa Ruangwa mkoani Lindi kisha dhidi ya Ruvu Shooting uliopigwa Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salam.

Afisa Habari na Mawasiliano KMC FC Christina Mwagala amesema kikosi chao kinafanya maandalizi yanayolenga kusahihisha makosa mbalimbali yaliyojitokeza katika maeneo, ambayo yalionekana kwenye michezo miwili iliyopita, na kupelekea Timu kukosa alama tatu muhimu.

“Tunajiandaa na mchezo ambao kimsingi utakuwa mgumu kutokana na kila Timu kuhitaji matokeo, tunawafahamu Mtibwa ni Timu nzuri na hata ukiangalia kwenye mchezo wao uliopita ambao wametoka sare walicheza vizuri na hivyo kama Timu tunajiandaa Ili kupata matokeo mazuri.”

“Ukiangalia kwenye mchezo ambao tulitoka sare na Ruvu Shooting wachezaji walicheza vizuri lakini bahati mbaya hatukupata matokeo mazuri lakini tunaamini ubora wa wachezaji wetu, umakini walionao utaleta matokeo chanya kwenye mchezo unaokuja kwasababu KMC tuna kikosi kizuri.” amesema Christina Mwagala

Hata hivyo hadi sasa KMC FC kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ipo katika nafasi ya tisa ikiwa na alama saba, baada ya kucheza michezo sita, ikishinda mchezo mmoja na kutoka sare michezo minne huko ikipoteza mmoja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live