Wakati Ligi ligi kuu ikisimama kwa muda kupisha michuano ya Kombe la Shirikisho, (ASFC), kocha mkuu wa KMC, Hitimana Thiery anakuna kichwa kuondoa mzimu unaoitesa timu hiyo kukosa matokeo mazuri ili kukwepa kushuka daraja.
KMC haijawa na mwenendo mzuri kwani tangu kuuanza mwaka 2023, haijashinda mchezo wowote katika mechi saba ilizocheza na kukaa nafasi ya 13 kwa pointi 23 baada ya kushuka uwanjani mara 24.
Timu hiyo ambayo kesho itakuwa uwanjani kukipiga na Mtibwa Sugar katika mchezo wa Kombe la FA kusaka nafasi ya kufuzu robo fainali, inakabiliwa na dakika 540 ngumu za kuamua hatma yao ya kubaki ligi kuu au kushuka daraja.
Katika mechi sita ilizobakiza itacheza mechi tatu nyumbani dhidi ya Kagera Sugar, Machi 9, Geita Gold na Singida BS, lakini pia ikitoka nje tatu dhidi ya Mbeya City, Prisons na Dodoma Jiji.
Thiery alisema pamoja na kukosa matokeo mazuri lakini bado anaendelea kusuka mbinu za kuhakikisha wanarejesha matumaini na furaha kikosini kwenye mechi zilizobaki.
Alisema wamepitia kipindi kigumu, lakini bado wanaamini KMC itatoboa na ishu ya kushuka daraja haitawagusa akiwaomba mashabiki kutulia na kuondoa presha akisema benchi la ufundi liko makini.
“Tunapitia kipindi kigumu japokuwa vijana wanapambana bahati ya kufunga mabao ndio haijapatikana, hatujakata tamaa na tunaendelea kupambana katika mechi sita zilizobaki ili kufufua matumaini mapya,” alisema kocha huyo.
Alisema kuwa kwa sasa ni kuwaandaa kisaikolojia vijana wake na kurekebisha makosa yaliyoonekana ili kuhakikisha wanarejea upya na kushinda mechi zilizobaki.