By RAMADHAN ELIAS KIKOSI cha KMC jana kilitua jijini Mwanza kwa ndege kujianda na mchezo wao wa Ligi Kuu raundi ya nane dhidi ya Yanga utakaopigwa Jumapili ya Oktoba 25 CCM Kirumba.
Wakati Yanga wakisafiri muda wowote kuanzia leo baada ya jana kucheza mechi yao ya sita dhidi ya Polisi Tanzania, wababe hao wa Kinondoni (KMC) tayari wameshawawahi jijini humo.
Kulingana na kanuni ya Ligi Kuu msimu huu inayoziruhusu timu kucheza mechi mbili za nyumbani kwenye viwanja tofauti itakavyovipendekeza timu husika, KMC imeuchagua Uwanja wa CCM Kirumba uliopo jijini Mwanza kama machinjio yao kwa Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Habibu Kondo ameahidi kuwapa burudani wana Mwanza.
“Wachezaji wote wapo tayari kwa mchezo tofauti na Sadala Lipangile ambaye bado hajawa fiti kwa asilimia mia lakini wengine wote wapo vizuri na tunaenda Mwanza kutoa burudani kwa mashabiki wetu wa Kanda ya Ziwa kwani ni muda mrefu umepita hatujacheza kule,” alisema.
“Kwakuwa sisi ndio wenyeji wa mchezo huo tumeamua kuwahi Mwanza ili wachezaji wazoee mazingira na uwanja. Utakuwa mchezo mgumu lakini tutapambana kuhakikisha tunaibuka na ushindi na kuwafurahisha mashabiki wetu,” alisema Kondo.