Chini ya Kocha Mkuu, Hitimana Thiery kikosi cha KMC kimepita kwenye dakika 630 za mateso kwa kukwama kusepana pointi tatu zaidi ya katika mechi 7 mfululizo.
Mechi moja pekee KMC iliambulia pointi moja kwenye sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar huku mechi tano wakiambulia kichapo mazima.
Kwenye msako wa pointi 21 ni pointi moja wamesepa nayo huku 20 zikiyeyuka jumjumla na safu yao ya ushambuliaji imefunga mabao manne huku ile ya ulinzi ikitunguliwa mabao 11.
Timu hiyo yenye maskani yake Kinondoni mara ya mwisho kupata ushindi ilikuwa ni Desemba 22,2022 iliposhinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania.
Kete zilizofuata zilikuwa ngumu kwa KMC ambapo ilishuhudia ubao ukisoma KMC 1-3 Simba, Desemba 26, 2022, Ihefu 1-0 KMC, Januari 3, 2023, Mtibwa Sugar 1-1 KMC, Januari 13, 2023.
KMC 1-3 Namungo, Januari 24, 2023,Ruvu Shooting 2-1 KMC, Februari 5, KMC 0-1 Yanga Februari 22 na Azam FC 1-0 KMC Februari 25.
Kibindoni imekusanya pointi 23 baada ya kucheza mechi 24 huku vinara wakiwa ni Yanga wenye pointi 62 baada ya kucheza jumla ya mechi 23.
Thiery ameliambia Championi Jumatatu kuwa wanahitaji kupata matokeo mazuri jambo ambalo wanalipambania na inawezekana kuwa hivyo kwa mechi zijazo.
“Hakuna anayependa kupata matokeo mabaya kwa mechi zetu za hivi karibuni zote zilikuwa ni ngumu ninawapongeza wachezaji wanazidi kuwa imara hivyo kwa mechi zijazo nina amini tutafanya vizuri”.