Mambo bado si shwari KMC baada ya juzi usiku kufikisha mechi ya nane mfululizo bila ushindi ilipolazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Geita Gold, licha ya nyota wa timu hiyo, Wazir Junior kuendelea kukifukuzia kiatu cha Mfungaji Bora msimu huu akifikisha mabao manane.
KMC ililazimishwa sare ya tatu mfululizo na ya sita katika mechi nane za Ligi Kuu Bara ilizocheza tangu iliposhinda mara ya mwisho Desemba 2, mwaka jana ikiifunga Mashujaa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam na kuifanya ifikishe pointi 25 kujikita nafasi ya tano kwenye msimamo.
Timu hiyo inayonolewa na Kocha Abdihalim Moallin ililazimika kusawazisha bao dakika ya 56 kupitia kwa Wazir akiunganisha kwa kicha krosi ya beki Raheem Shomary ambayo inakuwa ni asisiti yake ya tatu mfululizo katika ligi hiyo iliyopo raundi ya 19.
Geita ilitangulia kupata bao sekunde chache kabla ya mapumziko kupitia Yusuph Mhilu aliyemalizia pasi ya Tariq Seif na kuipa presha KMC ambayo katika mechi nane mfululizo ilizocheza bila ushindi, imejikuta ikipoteza michezo miwili kwa kufungwa na Azam (5-0) na Yanga (3-0), huku nyingine sita zikiisha kwa sare tofauti.
KMC ilitoka sare hizo tano dhidi ya Singida FG (0-0), Simba (2-2), Coastal Union (0-0), Namungo (2-2) na kufungana 1-1 mechi mbili mfululizo dhidi ya JKT Tanzania na Geita.
Bao la Wazir limemfanya afikishe manane na kulingana na Maxi Nzengeli wa Yanga, Marouf Tchakei wa Ihefu na Jean Baleke aliyekuwa Simba, pia mabao hayo yamezidi kumuweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuwania Kiatu cha Dhahabu kwani ni moja pungufu na aliyonayo Feisal Salum wa Azam mwenye tisa na mawili kabla ya kumfikia kinara Stephane Aziz KI wa Yanga anayeoongoza akiwa amefunga 10.
Mapema nyota huyo wa zamani wa Yanga, Dodoma Jiji na Toto Africans, alisema kiu yake ni kuhakikisha anatwaa kiatu cha ufungaji bora msimu huu.