Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KMC, Ihefu mambo safi, Biashara leo

34c5d5e8fea90f82c97fbd133774ebe6.jpeg KMC, Ihefu mambo safi, Biashara leo

Sun, 21 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

TIMU ya KMC na Ihefu FC zimenoga baada ya kushinda mechi za Ligi Kuu Tanznaia Bara jana.

KMC ikicheza kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es salaam ilishinda kwa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar, mabao mawili yalifungwa na Hassan Kabunda dakika ya 78 na 88 na Abdul Hillary dakika ya 16.

KMC imelipiza kisasi baada ya mchezo wa mzunguko wa kwanza kufungwa na Kagera bao 1-0 katika Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Ushindi huo unaifanya KMC kupanda nafasi moja kutoka ya sita hadi ya tano na kuwashusha Ruvu Shooting zote zikiwa na pointi 31 ila zikitofautiana kwa uwiano wa mabao ya kufungwa na kufungwa.

Huo ni ushindi wa pili mfululizo KMC inapata baada ya kuifunga Mwadui mabao 2-1 kwenye Uwanja huo huku Kagera ikitoka kupata sare ya mabao 3-3 dhidi ya Yanga.

Ihefu ilishinda mabao 3-2 dhidi ya Mwadui katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Highland Estate, Mbeya.

Kwa upande wa Ihefu mabao mawili yalifungwa na Omary Hassan dakika ya 59 na 72 na Andrew Simchimba dakika ya 21 huku ya Mwadui yakifungwa na Uhuru Selemani dakika ya 12 na Denis Richard dakika ya 56.

Ligi itaendelea leo kwa mechi mbili kuchezwa ambapo Biashara United itachuana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Karume, Mara na JKT Tanzania itawakaribisha Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Biashara huenda baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Simba kwa bao 1-0 ikatumia mchezo huo kumaliza hasira ila unaweza kuwa mgumu kwani Ruvu iliyotoka kushinda dhidi ya Gwambina inahitaji matokeo mazuri pia kulinda nafasi yake.

Kwa upande wa JKT imetoka kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania huenda ikatumia nguvu nyingi kutafuta ushindi na kujiondoa kuingia hatarini.

Lakini mchezo unaweza kuwa mgumu kwa kuwa Coastal imetoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Dodoma kwa mabao 2-1 itapambana kutafuta ushindi ikijua inaweza kuwa hatarini baadaye kutokana na nafasi waliyopo.

Chanzo: habarileo.co.tz