KIMENUKA Jangwani! Ile sare na Namungo imeshazua jambo pale Yanga.
Uongozi wa klabu ya Yanga umemlima barua straika wao kinara wa mabao, David Molinga ‘Falcao’ ya kumtaka ajieleze sababu za kukacha kufuatana na timu kule Lindi kuikabili Namungo ambako Wanajangwani walishikiliwa kwa sare ya tisa msimu huu.
Kwa mujibu wa barua hiyo, Molinga amepewa siku tatu za kujieleza kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu.
Imeelezwa katika barua hiyo kwamba kama atashindwa kutoa maelezo yenye mashiko, atapewa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine wa klabu hiyo.
Kabla ya mechi dhidi ya Namungo, kocha wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael aliwatuhumu baadhi ya wachezaji wake kuchagua mechi wakitaka wapangwe zile kubwa, kauli iliyoonekana kumlenga Molinga ambaye hakujumuishwa hata benchi katika Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba Machi 8.
Eymael alieleza kukerwa na wachezaji wanane ambao hawakwenda Lindi kuwakabili Namungo kutokana na sababu zao binafsi ambazo alisema hazikuwa na msingi.
Pia Soma
- Mzee Yusuf apata kigugumizi kufafanua ‘Narudi Mjini’
- Mkude aingia mitini kambini Taifa Stars
- Ndoto za Miraji Athuman zakatishwa kikatili Simba
Mbali na David Molinga wengine saba waliomkera Kocha ni Erick Kabamba, Paul Godfrey, Ramadhani Kabwili, Abdulaziz Makame, Raphael Daudi, Gustavo Simon na Adam Kiondo.
“Awali kuna maeneo machache nilitaka kuongeza wachezaji wapya lakini kwa jambo hili la utovu wa nidhamu ambalo limefanywa na wachezaji wangu limenifanya kuanza kutafakari na kufikiria upya jinsi ya kuiboresha timu kuwa na wachezaji ambao watatambua majukumu yao,” alisema.
“Lugha rahisi ya jambo ambalo walifanya wachezaji ambao hawakuja katika mechi ya Namungo bila sababu za msingi walitamani kuona timu inapoteza.”