Klabu ya Juventus inapanga kumpa njia Jadon Sancho ili aondoke Manchester United kwa mkopo Januari na inaweza kubadili dili na kumnunua jumla kwa Pauni 60 milioni itakapofika dirisha la kiangazi.
Miamba hiyo ina nia ya kumsajili winga huyo aliyewekwa kando kwa sasa baada ya kumjibu kocha wake Erik ten Hag kupitia akaunti yake ya X.
Sancho alitemwa kikosini kabla ya mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal mwezi uliopita, lakini Juventus imeibuka ikionyesha nia ya kuhitaji saini yake kwa mkopo kwanza.
Sakata la Sancho limetokana na Ten Hag kusisitiza mbele ya waandishi wa habari kwamba aliamuacha kikosini kwa sababu ya kutojituma mazoezini - lakini winga huyo alimjibu kocha wake kuwa anafahamu kwa muda mrefu alikuwa akifanywa kama mbuzi wa kafara.
Sasa winga huyo mwenye umri wa miaka 23 anafanya mazoezi nje ya kikosi cha kwanza baada ya kukataa kuomba msamaha na maisha yake ya Old Trafford yakielekea ukingoni kwa mujibu wa ripoti.
Borussia Dortmund ilikuwa ikipigiwa debe imrudishe mchezaji wao ambaye alikaa kwa muda wa miaka minne kabla ya kuhamia Man United kwa Pauni 73 milioni mwaka 2021.
Lakini vyanzo vya habari vinadai kuwa Sancho hataki kurudi Dortmund kwani anataka kujenga maisha yake upya huko Italia.
Mabosi wa Man United wanafahamu kuwa watapata hasara lakini kutokana mchakato unavyokwenda winga huyo huenda akaondoka katika dirisha dogo la usajili la Januari.
Wakati huo huo, mabosi wa Man United wanapanga kumwongeza Victor Lindelof mkataba wa miezi 12 mwezi ujao kwani Ten Hag amefurahishwa na kiwango chake na anafahamu wazi AC Milan na Juventus zinamnyemelea.