Benchi la Ufundi la Arsenal limemuongeza Beki kutoka Uholanzi Jurrien Timber kwenye kikosi chake cha Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kipindi cha pili cha msimu huu, huku akikaribia kurejea baada ya kupata jeraha baya.
Timber alijiunga na Arsenal akitokea Ajax kwa ada ya Pauni Milioni 38 wakati wa majira ya joto, lakini alipata jeraha baya wakati wa mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England, baada ya kufanyiwa upasuaji, aliachwa kwenye orodha ya kikosi cha Ulaya kwa hatua ya makundi.
Lakini Timber sasa amerejea kwenye kikosi, huku Mikel Arteta akimpa nafasi ya juu ambayo iliachwa na Lino Sousa aliyejiunga Aston Villa Januari 2024.
Makadirio ya awali ilikuwa mchezaji huyo pengine angekuwa nje kwa kipindi cha miezi saba hadi tisa na angerejea Machi, lakini sasa imeonekana nyota huyo atarejea pungufu ya muda huo.
Arsenal itamenyana na FC Porto katika hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini mechi hiyo itakuwa mapema sana kwa Timber.
Mechi ya kwanza imepangwa kufanyika Februari 21, na marudiano Machi 12.
Iwapo Arsenal wataendelea, wanaweza kumtumia Timber kwenye Robo Fainali, ambayo inatarajiwa kuanza Aprili 9 na kumalizika siku nane baadae.
“Kwa bahati mbaya, hilo ni jeraha la muda mrefu,” alisema Arteta.
“Anafanya vizuri sana lakini bado yuko mbali na kuwa fiti kufanya mazoezi na timu, au kitu cha kushindana na timu kwa hivyo hatutarajil atarejea hivi karibuni.”
Timber alianza msimu kama beki wa kushoto wa Arsenal, kwa sababu ya kukosekana kwa Oleksandr Zinchenko, lakini jeraha lake la kutisha mwishoni mwa juma la ufunguzi wa msimu lilimlazimu Arteta kufanya mabadiliko.
Takehiro Tomiyasu ambaye ni mahiri amesaidia upande wa kushoto nyakati fulani, kama vile mlinzi wa kati Jakub Kiwior, lakini kurejea kwa Timber kunaongeza matumaini ya Arsenal.