Jurgen Klopp ameondoka England baada ya kudumu Liverpool kwa misimu tisa na anahitaji kupumzika.
Klopp alisema ameushiwa nguvu ya kuendelea na kazi hiyo na sasa anaenda kutuliza akili baada ya kuichosha muda mrefu akisimamia mafanikio ya miamba hiyo Majogoo wa Liverpool na kwa moyo kunjufu klabu nzima na mashabiki wameridhika.
Licha ya Liverpool kutamani kuendelea kuwa naye, hakuna namna, siku moja angeondoka na hakuna marefu yasiyo na ncha.
Klopp anaacha mshahara wa Pauni 15 milioni kwa mwaka (zaidi ya Sh40 bilioni). Ni nyingi. Sasa anaenda kukaa tu kula bata. Hata hivyo, haoni shida. Anapata pesa nyingi kutokana na madili mengine na anaishi maisha ya kibosi kweli.
ANAPIGAJE PESA
KWA mujibu wa tovuti ya Celebrity Net Worth, Klopp ana utajiri unaofikia Dola 50 milioni.
Mbali na mshahara wake wa Pauni 15 milioni kwa mwaka ambao huongezeka kufikia Puni 20 hadi 25 milioni pamoja na nyongeza ya bonasi, Mjerumani huyu pia anapata pesa kupitia madili yake mengine ya nje ya uwanja.
Ni balozi wa kampuni ya New Balance, ambayo ndio inatengeneza jezi za Liverpool.
Pia mzee huyu ni balozi wa kampuni ya bia ya nchini kwao Warsteiner, kampuni ya utengenezaji wa magari ya Opel, mabingwa wa utengenezaji wa vifaa vya Kielektroniki Philips na TV network Sky Deutschland.
Kwa pamoja madili yake yote yanadaiwa kumpa karibia Euro 50 milioni kwa mwaka.
MSAADA KWA JAMII
Mwaka 2018 alitoa Pauni 4,000 kumpa Mkurugenzi wa michezo wa Liverpool aliyekuwa anajiandaa kwa ajili ya kushiriki mbio za kukusanya pesa kwa ajili ya kusaidia watu wenye kansa.
Aliwahi kushiriki kwenye mechi ya hisani iliyoandaliwa na James Milner kupitia taasisi yake ya James Milner Foundation mwaka 2018. Mapato ya mechi hii yalienda kusaidia watu wanaosumbuliwa na kansa.
Pia amekuwa akitoa pesa taasisi ya Liverpool Foundation inayomilikiwa na timu hiyo na anatajwa ametenga muda wa kutembelea hospitali ya Alder Hey mara kwa mara kuona watoto wenye ulemavu na watu wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali.
Klopp anatoa asilimia moja ya mshahara wake kwenda kwenye kampeni iliyoanzishwa na Juan Mata Common Goal initiative.
MJENGO
Juni 2022, alinunua nyumba Mallorca, Hispania kwa Pauni 3.4 milioni kutoka kwa kutoka kwa mfanyabiashara raia wa Uswiss Rolf Knie.
Mbali ya mjengo huo pia anamiliki nyumba Ujerumani.
Hata hivyo, muda mwingi kwa sasa huenda akautumia huko Hispania ili kupumzisha akili, nyumba hiyo ipo sehemu yenye mazingira ya fukwe.
NDINGA
1. Opel Insignia Dola 23,000
2. Audi A7 - Dola 72,000
3. Bentley Continental - Dola 370,000
MAISHA BINAFSI
Amewahi kuoa mara mbili na mkewe wa kwanza ni Sabine Klopp na waliachana mwaka 2001, kisha akamuoa Ulla Sandrock mwaka 2005 ambaye yupo naye hadi sasa.
Ana mtoto mmoja wa kiume aitwaye Marc Klopp ambaye alikuwa ni mchezaji kabla ya kustaafu mwaka 2015, kutokana na majeraha ya mara kwa mara yaliyokuwa yanamwandama. Marc aliwahi kuichezea Borussia Dortmund.