Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jumapili ina nini Yanga?

Dickson Job Kitasa Jumapili ina nini Yanga?

Sun, 12 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wanaanza kutupa karata ya kwanza katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi kwa kupambana na Union Sportive Monastirienne ya Tunisia.

Mchezo huo utachezwa leo Jumapili Uwanja wa Stade Olympique Hamadi Agrebi, huku Yanga ikiwa na kumbukumbu nzuri na mara ya mwisho ilipocheza iliifunga Club Africain bao 1-0 hatua ya mtoano.

Wakati kiu ya mashabiki wa soka nchini ni kuona timu zetu zinafanya vizuri kwenye michuano hii, ila Yanga imekuwa na bahati mbaya ya kuchezea vichapo kwenye mechi nyingi inapocheza Jumapili.

Kuthibitisha hilo Jumapili ya Oktoba 27, 2019 katika mchezo wake wa kwanza wa mtoano kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Pyramids ya Misri.

Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba mabao ya Pyramids yalifungwa na Eric Traory na Abdallah Saied huku la Yanga la kufutia machozi likifungwa na aliyekuwa nahodha wake, Papy Tshishimbi.

Mzimu wa kucheza Jumapili uliendelea kuitesa Yanga kwani mchezo wake wa marudiano uliopigwa jijini Cairo Novemba 3, 2019 ilifungwa pia mabao 3-0 na kutolewa rasmi kwa jumla ya mabao 5-1.

Jumapili ya Mei 6, 2018 ikiwa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika ilichezea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa USM Alger katika mchezo wa pili wa marudiano uliochezwa huko nchini Algeria.

Kichapo hicho kilikuwa ni cha kisasi kwa USM Alger ambao mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Dar es Salaam Jumapili ya Agosti 19, 2018 ilifungwa 2-1 kwa mabao ya Deus Kaseke, Heritier Makambo.

Mchezo mwingine kwa Yanga katika kundi hilo ulikuwa ni wa kichapo cha mabao 3-2 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, mechi iliochezwa Jumapili ya Julai 29, 2018 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ukiachana na Kombe la Shirikisho ambalo Yanga inashiriki ila hata kwenye Ligi ya Mabingwa nako imekuwa na nuksi inapocheza michezo yake siku ya Jumapili kwani mingi kati yake imepoteza pia.

Jumapili ya Septemba 12, mwaka 2021 ilijikuta ikishangazwa na River United ya Nigeria baada ya kufungwa bao 1-0 katika hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kama haitoshi mchezo wa marudiano uliopigwa Jijini Port Harcourt, Nigeria Jumapili ya Septemba 19, 2021 ilifungwa pia bao 1-0 na kuondoshwa rasmi Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 2-0.

Jumapili ya Oktoba 16, mwaka jana ilipoteza bao 1-0 dhidi ya Al Hilal kutoka Sudan katika mchezo wa awali wa mtoano kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kisha kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1.

Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa Oktoba 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga ilishindwa kutumia vyema faida za kucheza nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya kufungana 1-1.

Jumapili ya Machi 15, 2009 katika mchezo wa awali wa raundi ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ikicheza ugenini ilikubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Al Ahly ya Misri.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa International mjini Cairo, mabao ya wenyeji hao yalifungwa na nyota wake, Mohamed Barakat aliyefunga mawili huku lingine likifungwa na Flavio Amado.

Hata hivyo, matokeo hayo yalikuwa ni mlima mrefu kwa Yanga kwani haikuweza kupindua meza katika mchezo wa marudiano uliopigwa Aprili 14, 2009 jijini Dar es Salaam baada ya kufungwa tena bao 1-0.

MSIKIE LUNYAMILA

Nyota wa zamani wa Yanga aliyekuwa kwenye kikosi kilichoweka rekodi ya kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua hiyo mwaka 1998, Edibily Lunyamila anasema suala la kupoteza michezo mingi kwa siku hiyo kwake halichukulii kwa umakini mkubwa kwani anaamini jambo hilo limekaa kiimani zaidi.

“Tunatakiwa kuangalia wakati wanapoteza michezo siku hiyo walikuwa kwenye hali gani kwa sababu unaweza ukawahukumu ila kumbe hawakuwa bora zaidi ya wapinzani ambao walikutana nao,” alisema.

Chanzo: Mwanaspoti