Licha ya kwamba timu yake ipo nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, nyota wa Tanzania Prison, Jeremiah Juma ndiye mchezaji pekee aliyefunga mabao matatu kwenye mechi moja ‘Hat trick’ hadi sasa.
Jumaa alifunga Hat trick hiyo Novemba 27, mwaka jana kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC kwenye mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Nelson Mandela Sumbawanga na kumalizika kwa Prison kushinda mabao 3-1.
Juma ni miongoni kwa wachezaji walio kwenye mbio za kuwania kiatu cha mfungaji bora kwani hadi sasa amefunga jumla ya mabao matano.
Mbio hizo zinaongozwa na Reliants Lusajo wa Namungo mwenye mabao 10 akifuatiwa na George Mpole wa Geita Gold mwenye mabao nane huku Fiston Mayele wa Yanga akiwa nafasi ya tatu na mabao saba.
Juma na timu yake leo Saa 10:00 jioni watakuwa Uwanja wa wa Sokoine Mbeya, kucheza mechi yao ya kwanza ya duru ya pili ya LIigi dhidi ya watani zao Mbeya City.
Katika mechi 15 za duru ya kwanza Prison imevuna pointi 11 ikishinda mechi tatu tu, sare mbili na kuopoteza 10 huku ikiwa imefunga jumla ya mabao nane na kuruhusu mabao 20.