Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Julio: Singida mbona Timu ipo, subirini maajabu

Jamhuri Kihmelu Julio.jpeg Jamhuri Kihwelu ‘Julio’

Sun, 17 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kuanza na ushindi katika mchezo wake wa kwanza akiwa na kikosi cha Singida Fountain Gate, kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio' ameichambua timu hiyo na kuanika kilichosababisha ifanye vibaya na kutopata ushindi katika mechi za Ligi Kuu kwa takribani miezi mitatu na siku 18 tangu Novemba 27, mwaka jana.

Julio ambaye amejiunga na timu hiyo Machi 12, mwaka huu akichukua mikoba ya Thabo Senong juzi aliisaidia kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa akiwa na siku tatu tangu ajiunge na kikosi hicho.

Akizungumza jijini hapa, Julio alisema kwamba kwa siku tatu alizokaa na wachezaji wa timu hiyo alibaini kwamba walikuwa wamekata tamaa na walikuwa hawafanyi mazoezi kwa usahihi jambo ambalo lilichangiwa na wachezaji wenzao saba kutimkia Ihefu dirisha dogo.

Alisema kitu cha kwanza alichoanza nacho ni kuwajenga kisaikolojia kurudisha hali ya upambanaji na kujituma, kujenga morali na kuwaaminisha kwamba wanaweza, jambo ambalo limemlipa matunda katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Namungo.

"Singida Fountain Gate siyo timu mbaya, tatizo la vijana ni kuwa kuna wachezaji wametoka kwenda Ihefu kwahiyo morali ikashuka, lakini na mazoezi yale ya nguvu kuwafanya wawe fiti nayo wakawa hawafanyi vizuri, siku tatu zangu za mwanzo nimejaribu kusukuma hicho kitu na wasaidizi wangu," alisema Julio na kuongeza;

"Kazi kubwa tuliyokuwa nayo ni kuwajenga kisaikolojia na kufanya uhamasishaji kwa sababu tukisema tumefanya nao kazi kubwa sana ndiyo maana tumepata ushindi utakuwa ni uongo,"

"Lakini siku tatu za mazoezi tumejaribu kusisitiza tulichoona kinapungua lakini kingine kuwajenga sana saikolojia na kupandisha morali na kuwaambia wao wana uwezo mkubwa wanatakiwa wafanye kazi, tunamshukuru Mungu wameweza kufanikisha hilo," alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Dodoma Jiji, Namungo na KMC, aliwapongeza wachezaji wake kwa kujituma na kupata ushindi huo mbele ya timu ngumu ya Namungo, huku akijiweka mtegoni kwa kuahidi mwendelezo wa matokeo mazuri na kuisaidia timu hiyo kurejea katika nafasi za juu kwenye ligi.

Chanzo: Mwanaspoti