Aliyewahi kuwa mchezaji na Kocha wa Simba, Jamhuri Julio Albeto amesema kuwa Klabu ya Azam ndiyo timu yenye nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara lakini inashindwa kutokana na viongozi wake kuendekeza majungu badala ya mpira.
Julio ambaye amewahi pia kuzifundisha Namungo na Taifa Stars amesema kuwa endapo akikabidhiwa timu hiyo, atachukua ubingwa huo 'back to back' kwa miaka 10 mfululizo.
Kocha huyo amesema anaamini Azam FC ni timu yenye sifa za kipekee nchini Tanzania, na imekua ikidhihirisha hilo kwa vitendo, lakini inakwama kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara.
Azam FC tangu imeanzishwa mwaka 2004, imetwaa ubingwa wa Tanzania Bara mara moja, msimu wa 2013/14 ikiipiku Young Africans iliyokuwa Bingwa msimu mmoja nyuma.
“Azam ndio Timu iliyosajili Wachezaji wazuri tena kwa Hela nzuri sana lakini wanafeli kutokana na kutokuwa na Viongozi wa Mpira, wengi wao wanakalia majungu ukiacha Poppat.
“Ile Azam mfano nikipewa mimi niifundishe nikaenda na jopo langu la waalimu nakuahidi inabeba ubingwa miaka 10 mfululizo” Jamhuri Julio Albeto aliyewahi kuwa Kocha wa Simba, Namungo na Taifa Stars.