Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jude Bellingham sio Zidane wala Beckham

Jude Bellingham El Classico Jude Bellingham sio Zidane wala Beckham

Sat, 9 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Namna maisha yanavyokwenda kasi. Florentino Perez atakuwa mmoja kati ya watu wanaoshangaa namna maisha yanavyokwenda. Katika umri wa miaka 76 ameona mambo mengi maishani mwake. Kazi yake kubwa ni mhandisi.

Ameona namna ambavyo wakati fulani majengo ya Ulaya yalivyokuwa marefu zaidi duniani. Namna yalivyokuwa yanapendeza nyakati hizo. Ghafla majengo ya Bara la Asia yamekuwa majengo marefu zaidi duniani. Nyakati zinabadilika.

Halafu atarudisha mawazo yake katika soka. Ndiye tajiri wa Real Madrid. Nadhani atakuwa ameona mambo mengi yanavyobadilika katika soka akiwa katika kiti chake cha enzi anapokaa katika Uwanja wa Santiago Bernabeu akiwa na marafiki zake wa karibu.

Atakumbuka namna alivyovunja rekodi ya uhamisho kwa kumnunua Zinedine Zidane mwaka 2001. Dunia ilipigwa na butwaa. Bosi wa Juventus, Luciano Moggi alipigwa na butwaa wakati alipoambiwa na Perez : “Hakuna mchezaji asiyeuzwa duniani inategemea na kiasi gani cha pesa ulichonacho.”

Perez akamnunua Zidane. Bonge la mchezaji. Kipaji asilia. Alijua namna ya kuupaka mafuta mpira. Alikuwa pia mchezaji wa matokeo uwanjani. Bonge la kipaji. Ni masalia ya mwisho mwisho ya wachezaji walioujua kuuchezea mpira wakiwa peke yao kabla ya kucheza kitimu.

Baadaye Perez akamnunua David Beckham kutoka Manchester United. Ulikuwa uhamisho ulioshangaza wengi. Beckham? Ilionekana kama angekuwa na maisha marefu Old Trafford kutokana na umaarufu wake ambao ulikuwa unailetea Manchester United pesa nyingi achilia mbali uwezo wake wa kupiga krosi.

Waingereza walimtengeneza Beckham kuwa staa. Na alipoanza uhusiano wa kimapenzi na Victoria Adams basi Waingereza waliwatengeneza zaidi kiasi cha kuwapigia kura mawazo ya kijinga kwamba sura zao zilipaswa kuwekwa katika noti zao.

Perez alipopata zali la kumnunua Beckham alikuwa anamnunua mtu ambaye alikuwa maarufu katika sura ya dunia kuliko wachezaji mahiri aliokuwa nao ambao walikuwa na uwezo mkubwa kuliko Beckham. Akina Zidane, Ronaldo de Lima, Roberto Carlos, Luis Figo na Raul Gonzalez.

Lakini leo Perez ana mchezaji anayeitwa Jude Bellingham. Maisha yanakwenda kasi. Jude amehamia Madrid kwa kiasi cha Pauni 88 milioni tu akitokea Borussia Dortmund. Anaweza kuwa mchezaji muhimu zaidi katika kikosi cha Real Madrid kwa sasa.

Mpaka sasa Jude ndiye mchezaji aliyewahi kuifungia Real Madrid mabao mengi zaidi ndani ya mechi 15 za kwanza. Hakuna mchezaji aliyewahi kufanya hivyo. Hata Cristiano Ronaldo hakuwahi kufanya hivyo alipoanza kuvaa jezi ya Madrid.

Lakini pia Jude amechangia mabao 19 katika mechi zake 17 za kwanza Real Madrid. Perez atakuwa anakuna kichwa chake na kushangaa namna zama zinavyobadilika. Perez ana bahati ya mtende. Amefanikiwa kuona mabadiliko ya soka la kisasa na amepata wanasoka wa kisasa.

Jude anamfikia Zidane kwa umahiri na kipaji maridadi mguuni? Hapana. Anazidiwa na wengi. Anazidiwa na akina Andres Iniesta, Jay Jay Okocha, Ronaldinho, Andrea Pirlo na wengineo wengi. Lakini soka la kisasa haliwahitaji tena kina Ronaldinho. Linawahitaji wachezaji kama Jude na bahati nzuri Perez anaye katika timu yake.

Soka la kileo linahitaji wachezaji wanaokimbia kilomita nyingi uwanjani na kufanya majukumu mengi. Unaweza kuwa kiungo mahiri lakini unahitajika kukaba, kupasia kwa haraka na kutimiza majukumu mengi ambayo unapewa na kocha kuliko kuonyesha uwezo wako binafsi kama kina Zidane.

Na hapa hapa katika kukimbia huku na kule ndipo unapomkuta mchezaji kama Jude ana mabao mengi katika mechi 15 za kwanza za Real Madrid kuliko mchezaji mwingine yeyote katika historia ya klabu hiyo. Majuzi nilikuwa namsikia Caro Ancelotti akielezea tofuti kati ya Zidane na Jude.

Kwamba Jude ni mchezaji wa kisasa anayekimbia kilomita nyingi uwanjani wakati Zidane alikuwa ni mchezaji mwenye ubora binafsi zaidi. Ni kweli. Katika zama hizi inawezekana kuna wachezaji kama Zidane lakini aina ya soka la kisasa haimruhusu kuonyesha ubora wake.

Lakini hapo hapo lazima tukumbuke Perez atakuwa anawaza namna ambavyo maisha yamekwenda kasi kwa upande wake. Ana Jude mkononi lakini Jude sio David Beckham. Jude sio mchezaji wa biashara wala mchezaji ambaye amepambwa sana na ndugu zake.

Huyu ni mchezaji ambaye hajakuzwa na uhusiano wa mapenzi wala hajatengenezwa na soka la Kiingereza. Alienda kukomaa zaidi akiwa Dortmund. Zamani asingefaa katika wasifu aliokuwa anautaka Perez. Kwa zama hizi huyu asingekuwa Galacticoz.

Hajanunuliwa kwa sababu ya mauzo ya jezi. Lakini ni wachezaji wangapi wa kisasa ambao katika zama hizi unaweza kuwanunua kwa mauzo ya jezi? Sidhani kama kama kina Erling Haaland unaweza kuwanunua kwa ajili ya mauzo ya jezi. Labda Kylian Mbappe.

Jude hajatengenezwa kibiashara. Hajatengenezwa kwa mwonekano aonekane staa. Anafanya tu kazi yake kama wachezaji wengi wa sasa wanavyofanya kazi zao bila ya kupambwa sana na vyombo vya habari. Ni kama ilivyokuwa kwa Wayne Rooney. Jude hana mvuto wa kibiashara lakini ndio wachezaji ambao Perez aliwahitaji katika soka la kisasa kama alitaka mabadiliko katika klabu yake.

Mfano ni wachezaji wa Manchester City au Liverpool ambao katika miaka ya karibuni wametawala soka la ulimwengu. Hawakuwa na majina makubwa wala mvuto mkubwa wa kibiashara lakini wamefanya kazi zao kwa ufasaha.

Ndicho ambacho kinatokea Arsenal kwa sasa. Haina wachezaji wenye mvuto wa kibiashara ulimwenguni lakini wanajaribu kufanya kazi yao kwa ufasaha. Hapo ndipo unapomsifu Perez kwa kuwa na Jude. Sio Zidane wala sio Beckham lakini ndiye mchezaji anayehitajika katika zama hizi za kisasa.

Chanzo: Mwanaspoti