Meneja wa Real Madrid Carlo Ancelotti amemwaga sifa kiungo wake mpya, Jude Bellingham baada ya kucheza mechi yake ya kwanza na kuwaambia wachezaji wengine wanapaswa kuiga ubora wa staa huyo.
Kiungo huyo Muingereza aliingia uwanjani kwenye mechi akiwa mchezaji wa Madrid kwa mara ya kwanza wakati Los Blancos walipokipiga na AC Milan kwenye mechi ya kirafiki na kushinda 3-2. Bellingham alicheza dakika 64 kwenye mechi hiyo.
Mechi hiyo iliyofanyika uwanjani Rose Bowl huko California ilikuwa burudani tosha kwa mashabiki, ambapo Real Madrid ilitokea nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda.
Kwa wachezaji wa ndani kwenye mechi hiyo ni Bellingham na Fede Valverde pekee ndiyo waliorejea uwanjani kwenye kipindi cha pili, kisha Valverde akafunga mara mbili kabla ya Vinicius Jr kutupia nyavuni bao la ushindi.
Hata hivyo, Bellingham ndiye aliyemvutia kocha Ancelotti zaidi na kusifu usajili wake huo wa Pauni 115 milioni kwa kucheza kibabe sana kwenye fomesheni mpya ya 4-3-1-2.
“Nimependa (fomesheni mpya),” alisema Ancelotti na kuongeza: “Kuna vitu lazima uviboreshe kidogo. Ilikuwa ngumu sana kwetu kutokea nyuma.
Tulijaribu kucheza ndani zaidi kuliko nje. Nafasi ya Bellingham ilikuwa nzuri na alikuwa na mechi nzuri, wachezaji sasa itabidi waendane na ubora wake. Lazima tufurahie ujio wake.”
Ancelotti aliendelea kusema kwamba: “Ni nadra sana kupata wachezaji wenye ubora kama ule na kitu cha kustaajabisha pia kukipata kwa mchezaji wa miaka 20.
“Bado ana nafasi ya kuwa bora zaidi, lakini kubwa tumekuwa na bahati kuwa hapa kwetu.”
Bellingham ni kiraka, anaweza kucheza nafasi tofauti kwenye safu ya kiungo, ambapo kwenye mechi hiyo ya AC Milan, alicheza nyuma ya mshambuliaji wa kati kama Namba 10.