Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Joto la 2024/25, nahodha Yanga ashtukia jambo

Yanga Mpyaaaaaaaaa.jpeg Joto la 2024/25, nahodha Yanga ashtukia jambo

Fri, 12 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi ufukweni ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano, huku nahodha msaidizi wa timu hiyo, Dickson Job akishtukia jambo na kusema wamerudi vizuri, ila safari hii wanatarajia kupata ugumu zaidi msimu ujao kutokana na timu pinzani zitakavyowatolea macho.

Hata hivyo, Job amesema licha ya kutarajia ugumu huo, bado anaamini kwa usajili uliofanywa na klabu hiyo kuongeza majembe ya maana, msimu ujao ‘patachimbika’ kwani hata hao hawatakubali kirahisi.

Job amefunguka hayo muda mchache baada ya timu hiyo kuanza kambi jijini Dar es Salaam ambapo juzi na jana walikuwa Ufukwe wa Coco, huku akikiri ubora waliouonyesha msimu uliopita utaongezeka zaidi kutokana na maingizo mapya.

“Benchi la ufundi liliona upungufu ndio maana wameongeza nguvu katika baadhi ya maeneo hivyo, ujio wa wachezaji wapya utaongeza changamoto kwa wachezaji wenyewe kwa wenyewe na kuleta chachu ya ubora wa kikosi,” alisema Job na kuongeza;

“Natarajia msimu mwingine bora na wa ushindani kilichopo sasa ni sisi wachezaji kujiweka fiti tayari kwa mapambano kazi ya viongozi imefanyika benchi la ufundi na wachezaji ni wakati wetu kuhakikisha tunatetea taji, kwani tunajua wapinzani watatutolea macho kuliko msimu uliopita.”

Job alisema wamewakaribisha wachezaji wote wapya na wamezungumza nao kuwa malengo yao ni kutetea mataji yote hivyo wanatakiwa kuungana nao kuhakikisha wanafikia malengo.

“Ujio wa mastaa wapi na sisi tulioendelea kuwepo tuna deni kubwa la kufanya ili tuweze kufikia malengo natambua uwezo wa mastaa waliokuja mfano Clatous Chama ni kiungo ambaye anarahisisha mambo uwanjani, Prince Dube ni mzuri kwenye guona goli kazi yetu ni kuhakikisha pasi zinawafikia,” alisema Job na kuongeza;

“Mimi kazi yangu ni kukaba kuhakikisha namlinda Djigui Diarra lakini naomba kuwahakikishia wananchi kuwa usajili uliofanyika kukiwa na mwamba wa Lusaka msambazaji wa pasi za upendo ambaye ukimpa pasi atakama ilikuwa mbaya anaifanya kuwa nzuri ntafunga tena.”

Job ambaye ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza kuifungia bao Yanga msimu uliopita ametamba kuwa msimu ujao atafunga mabao zaidi ya mawili, huku akitamba kuwa kati ya mabao hayo litapatikana bao bora la msimu.

Akizungumzia maandalizi kwa ujumla alisema wachezaji wote wapo vizuri kwani asilimia kubwa kati yao walikuwa na mechi za hisani hivyo wamerudi wakiwa kwenye utimamu sasa wanajifua mdogo mdogo.

“Kwa asilimia kubwa wengi wetu tumekutana kwenye matamasha ya hisani na wengine tulikuwa tunafanya mazoezi pamoja lakini wageni tumewakaribisha na kuwaeleza malengo yetu na wao pia wanatambua Yanga ni timu ya mataji tunataka mataji msimu ujao.”

Kwa misimu mitatu Yanga imekuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA), mbali na kutwaa Ngao ya Jamii mara mbili na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni baada ya kupita miaka 25 ilipocheza mara ya kwanza 1998.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: