Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Joselu, shabiki hadi shujaa Madrid

Frdxdxx Joselu, shabiki hadi shujaa Madrid

Fri, 10 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Miaka miwili iliyopita, Mei 28, 2022, jijini Paris, Ufaransa, alikuwa na baba yake kutazama fainali ya Ligi ya Mabingwa kati ya Real Madrid na Liverpool.

Picha za Selfie alizopiga nje ya uwanja wa Stade de France zilimuonyesha akiwa amevaa jezi ya Madrid ikiwa ni ishara ya kushabikia chama hilo.

Hata hivyo, usiku wa juzi Jumatano, Jose Luis Mato Sanmartin ‘Joselu’ alikuwa shujaa akiwa na uzi wa Madrid.

Ni miaka miwili tu, imebadili kila kitu kwenye historia ya Joselu ambaye kuna timu zikimkumbuka zinaweza kububujikwa na machozi.

Hizi ni Stock City na Newcastle na huko alionekana si lolote na alikalia benchi na hakuwa na madhara kwenye mechi za timu hizo.

Mabao mawili aliyofunga kwenye mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich kwenye ushindi wa mabao 2-1 uliipeleka Madrid fainali akiwa na umri wa miaka 34. Ndoto imetimia akiwa na chama lake hilo.

Joselu kwa sasa anacheza kwa mkopo Madrid akitokea Espanyol aliyojiunga nao dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana na amefunga mabao 17 ya michuano yote huku matano kati ya hayo ikiwa ni ya Ligi ya Mabingwa.

Akiwa kijana kwenye miaka ya 20, Joselu aliwahi kucheza timu za vijana za Madrid na alipandishwa timu ya wakubwa na alicheza mechi mbili tu na baada ya hapo alitolewa kwa mkopo Celta Vigo kabla ya kuuzwa TSG Hoffenheim alikocheza msimu mmoja kisha akatolewa kwa mkopo Eintracht Frankfurt kisha akauzwa kwa Hannover 96 ambako alifunga mabao 14 na Stoke City ikalipa Pauni 5.7 kumnunua mwaka 2015.

Akiwa Stoke mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa kwani alifunga mabao manne tu na akawa anasugua benchi kabla ua msimu uliofuatia kutolewa kwa mkopo kwenda Deportivo La Coruna.

Huko pia hakukaa, Newcastle ikamrudisha England na ikatoa Pauni 5 milioni kumsajili lakini mambo yakawa yale yale kwani alifunga mabao saba tu katika mechi 52.

Baada ya misimu miwili ndani ya Newcastle alirudi alikozaliwa Hispania alipojiunga na Alaves mwaka 2019 na ndani ya misimu mitatu alifunga mabao 10 na zaidi.

Mwaka 2022 alitua Espanyol ikiwa ni muda mchache baada ya kutazama fainali ya Madrid na Liverpool, akiwa hapo akafunga mabao 17 katika mechi 37 za michuano yote lakini mabao 16 kati ya hayo ilikuwa ni ya La Liga.

Baada ya msimu kumalizika tu, Madrid ikapiga simu na kulipa Euro 500,000 kwa ajili ya kumsajili kwa mkopo wa msimu mmoja na zaidi walihitaji aende kuwa mbadala katika eneo la ushambuliaji ikiwa wachezaji wao tegemeo wataumia.

Mechi nyingi amekuwa akianzia katika benchi akiwa ameanza katika mechi 13 tu za La Liga ingawa mara zote ambazo anapata nafasi amekuwa akionyesha ubora wake katika kufunga.

Taji la Spanish Super Cup, ndio ambalo Madrid ilishinda mapema mwaka huu ndio lilikuwa lakwanza kwake katika maisha ya soka la kulipwa kwa upande wa klabu, likafuatia na La Liga na sasa anatazamia Ligi ya Mabingwa.

Chanzo: Mwanaspoti