Mshambuliaji mkongwe wa Kispaniola, José Luis Sanmartín Mato ‘Joselu’ usiku wa jana ametokea benchi na kuifungia mabao mawili Real Madrid ikitoka nyuma dakika tatu za mwisho na kushinda 2-1 dhidi ya Bayern Munich katika mchezo wa marudiano wa Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Santiago Bernabéu Jijini Madrid, Joselu (34) aliingia dakika ya 81 kuchukua nafasi ya kiungo wa Kimataifa wa Uruguay, Federico Santiago Valverde wakati huo Bayern Munich ikiongoza 1-0 kwa bao lililofungwa na beki Mcanada, Alphonso Boyle Davies (23) mwenye asili ya Ghana dakika ya 68.
Joselu akafunga bao la kusawazisha dakika ya 88 na la ushindi dakika ya 90'+1 akimalizia kazi nzuri ya beki Mjerumani mwenye asili ya Sierra Leone, Antonio Rüdiger.
Kwa matokeo hayo, Real Madrid ya kocha Mtaliano, Carlo Ancelotti (64) inakwenda Fainali kwa ushindi wa jumla wa 4-3 kufuatia sare ya 2-2 kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita Jijini Munich.
Sasa Real Madrid itakutana na Borussia Dortmund ya Ujerumani katika Fainali ya UEFA Champions League Jumamosi ya Juni 1, Mwaka huu Uwanja wa Wembley Jijini London ya Juni 1 mwaka huu.
Borussia Dortmund imefanikiwa kuingia Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuitoa Paris Saint-Germain ya Ufaransa kwa jumla ya mabao 2-0 ikishinda 1-0 nyumbani na ugenini.